TFF imulike mechi za lala salama FDL

Muktasari:

Ligi hiyo ya FDL imekuwa na msisimko mkubwa kwa wale wanaoifuatilia ingawa imekuwa haitangazwi sana tofauti na Ligi Kuu Bara ama hata ile Ligi Kuu ya Wanawake, labda pengine kwa vile haina wadhamini kama ilivyo kwa Ligi Daraja la Pili (SDL).

LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) imemaliza duru lake la kwanza na wikiendi ijayo inatarajiwa kuanza ngwe ya pili kabla ya kufungwa kwa pazia la msimu wa 2018-2019.

Sio siri ligi hiyo ya FDL imekuwa na msisimko mkubwa kwa wale wanaoifuatilia ingawa imekuwa haitangazwi sana tofauti na Ligi Kuu Bara ama hata ile Ligi Kuu ya Wanawake, labda pengine kwa vile haina wadhamini kama ilivyo kwa Ligi Daraja la Pili (SDL).

Tayari kuna baadhi ya timu zimeshasoma ramani katika mibio zao za kuwania nafasi za kupanda Ligi Kuu msimu wa 2019-2020 na viroho vimeshaanza kuwadunda wakati wakielekea kucheza mechi zao za duru la pili wiki ijayo.

Ukiangalia misimamo ya makundi mawili ya ligi hiyo kuna baadhi ya timu zimeonyesha kiu ya kutaka kupanda daraja, Namungo FC, Boma FC, Geita Gold FC, Mbeya Kwanza ni kati ya zilizofanya vyema kwenye mechi zao za duru la kwanza na kama itazichanga karata zao kwa mechi za duru lijalo zinaweza kufanya kuandika rekodi.

Miongoni mwa timu hizo hazijawahi kucheza kabisa Ligi Kuu hivyo kama zitapanda itakuwa ni faraja kwao na rekodi katika soka la Tanzania.

Kwa namna ushindani ulivyo kwa makundi yote mawili, Mwanaspoti ilikuwa inatoa angalizo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na hasa Bodi ya Ligi (TPLB) kujipanga mapema kwa ajili ya kuzimulika mechi hizo za mwisho kwa jicho la tatu.

Hatua iliyofikiwa kwa ligi hiyo yaani ngwe ya lala salama huwa na ushindani zaidi na ndipo kunakoelezwa hufanyika mipango mingi kwa klabu shiriki katika kuhakikisha zinazotaka kupanda Ligi Kuu zinafanikiwa, huku zile zinazoepuka kushuka daraja.

Kwani tayari kumekuwa na manung’uniko ya chini chini kwa baadhi ya mechi hasa suala la waamuzi, japo sio kwa kiwango kilichokuwa msimu uliopita.

Hata kama lawama na manung’uniko ya msimu huu hayalingani na yale yaliyowahi kuwepo kwenye mechi za ligi hiyo misimu miwili iliyopita, lakini ni vema TFF ikawa macho hivi sasa.

Waamuzi wamekuwa wakilalamikiwa kuzibeba timu wenyeji kwenye mechi zilizopita, hata kama sio kwa timu zote, lakini kinga ni bora kuliko tiba.

Lazima TFF iwe wakali na kufuatilia kwa ukaribu mechi za raundi hizo zilizosalia ili kuepusha hujuma zozote zinazoweka kutokea.

Kwa kuwa tungependa kuona timu zikipanda daraja hadi Ligi Kuu kihalali ndio maana Mwanaspoti inaikumbusha TFF kuwa macho kwa kuchelea kilichowahi kutokea katika ligi hiyo misimu miwili iliyopita.

Kuwepo kwa manung’uniko na lawama kwa TFF ni kutokana na vurugu zilizojitokeza mwishoni mwa msimu na kushuhudia baadhi ya timu zilizokuwa katika nafasi kubwa ya kupanda daraja zikikosa nafasi hiyo.

Kadhalika tunazikumbusha timu zote kuanzia mabenchi yao ya ufundi, wachezaji na hata viongozi na mashabiki wasiwe chanzo cha kutaka kuharibu mechi za raundi zilizosalia.

Inawezekana klabu zikafanya makusudi ama kwa kuanzisha vurugu au kuwageuza waamuzi kama chaka la kufichia udhaifu wa timu zao.

Wahakikishe kwa ushirikiano wao na wasimamizi wa ligi hiyo mechi zinachezwa na kumalizikakwa amani na utulivu, huku kila timu ikiyakubali matokeo itakayoyapata kwani asiyekubali kushindwa sio mshindani.

Kimsingi na ndicho kikubwa kwa vyote kwamba, mtu hupanda na huvuna kile anachokipanda na si vinginevyo, hivyo huwezi kulazimisha matokeo.

Pia timu zicheze mechi zao kwa kuamini kuwa soka huwa lina matokeo matatu, kufungwa, kushinda na kutoka sare na isitake kulazimisha matokeo ili kujinufaisha na kugeuka kuwa chanzo cha vurugu ambazo hazitasaidia kwa maendeleo kwa soka letu. Kocha wa Arusha United, Fred Felix aliwahi kusema Ligi Kuu ni nyepesi kuliko hii SDL.

TFF/TPLB kazi kwenu, sisi tumekumbusha tu!