TFF, mastaa wafunguka kifo cha Mzee Mkapa

Muktasari:

Rais wa TFF, Walace Karia amesema amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa.

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetuma salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Rais wa TFF, Walace Karia amesema amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa.

“Katika mpira wa miguu Mkapa ataendelea kukumbukwa siku zote akiacha kumbukumbu ya kujenga Uwanja wa Taifa ambao unafahamika kama Uwanja wa Benjamn Mkapa. Uwanja huu unatufanya kutembea kifua mbele katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika.

Mbali na TFF, wadau wa michezo na wachezaji nao wameeleza kusikitishwa na kifo cha Mzee Mkapa huku wakitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kufikisha salama hizo kwa ndugu na jamaa.

Straika wa FC Platinum ya Zimbabwe, Elias Maguli kupitia akaunti yake ya Instagram ameandika “Ni pigo kwa Taifa kumpoteza Mzee wetu Benjamin William Mkapa.”

Klabu ya AS Roma ya Italia kupitia akaunti ya Twitter wameandika “Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Mhe! Benjamin William Mkapa. AS Roma inatoa pole kwa familia yake, ndugu zake, marafiki na Taifa la Tanzania kwa ujumla”.

Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima pia ameandika “Inalilah wa iniilah rajiuni, rest in paradise babapole pia kwa wa Tanzania wote”

Beki wa kulia wa Yanga Paul Godfrey maarufu Boxer ameandika: “Mbele yake nyuma yetu”

Nahonda msaidizi wa Yanga Juma Abdul ameandika “Ukapumzike kwa amani mzee wetu inshaallah”

Straika Adam Salamba ameandika R.I.P mzee wetu”

Mrisho Ngassa ameandika “R.I.P mzee wetu”

Haji Mwinyi Mgwali ameandika “Mungu akupe kauli thabit kiongozí”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Mohamed Dewji (MO) ameandika: “Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un. Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwa hakika kwake Yeye tutarejea Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, jina la Bwana Lihimidiwe”

Klabu ya Mtibwa Sugar imeandika “Pumzika kwa amani Mh. Benjamin William Mkapa. “

Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara ameandika “Nimehemewa, Poleni Watanzania wenzangu”

Uongozi wa Timu ya Polisi Tanzania umeandika “Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia Julai 24, 2020. Polisi Tanzania FC tunatoa pole kwa Ndugu, Jamaa, Marafiki na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa.”

Uongozi wa Kagera Sugar wameandika: “Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mzee Benjamin William Mkapa, uongozi unatoa pole na salamu za rambirambi kwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli. Na pia Tutatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu mzito wa kuondokewa na mpendwa wetu”

Azam Football Club Limited wao wameandika “Tumepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa.Mkapa atakumbukwa kwa mambo mengi katika ulimwengu wa michezo, ikiwemo zawadi ya Uwanja wa Taifa ambayo alituachia Watanzania.

 

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ikimnukuu Rais John Magufuli imeeleza kuwa Rais mstaafu Mkapa alikuwa amelazwa jijini hapa.

Kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa tuendelee kumuombea mzee wetu ambaye ametangulia mbele za haki,” amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwa wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito.

 

KUHUSU MZEE MKAPA

Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 1938 wilayani Masasi mkoani Mtwara, ambapo aliiongoza nchi kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1995-2005.

Kiongozi huyo atakumbukwa kwa sera yake ya Uwazi na Ukweli na katika utumishi wake ikiwemo kusimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi. Aliweka mkazo katika ukusanyaji wa kodi ili kuwezesha Taifa kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuendelea miradi mikubwa ya maendeleo.