TFF, TPLB wachunguze kamati ukaguzi wa viwanja

HIVI karibuni viwanja viwili vya soka vilifungiwa kutumika kwenye mechi zozote za ligi zilizo chini ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutokana na kukosa viwango vya kuchezea.

Viwanja hivyo ni Uwanja wa Gwambina unaotumiwa na timu ya Gwambina FC yenye makazi wilayani Misungwi na Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume unaotumiwa na Biashara United ya mjini Musoma.

Uwanja wa Gwambina ulianza kufungiwa ukiwa umetumika kucheza mechi moja ya Ligi Kuu Bara huku Uwanja wa Karume ukiwa umetumika kuchezea mechi mbili.

TPLB walitoa uamuzi huo baada ya kugundua kwamba viwanja hivyo eneo la kuchezea na vyumba vya kubadilishia nguo kutokidhi viwango vilivyoanishwa kikanuni, hivyo kuwapa muda wa siku 21 kufanya marekebisho hayo.

Timu zote mbili zilielekezwa kwamba mechi zao zichezwe kati ya Uwanja wa Nyamagana ama CCM Kirumba - viwanja vyote vikiwa jijini Mwanza mpaka hapo marekebisho yatakapofanywa na kamati kujiridhisha juu ya marekebisho hayo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina kamati ambayo hufanya ukaguzi wa viwanja vyote ambavyo vinatumika kuchezea mechi za ligi mbalimbali ili kujiridhisha na endapo wanakuwa wamejiridhisha, basi huvipitisha viwanja hivyo kwa ajili ya matumizi husika.

Miongoni mwa maeneo ambayo yanapewa kipaumbele ni eneo la kuchezea (pitch), vyumba vya kubadilishia nguo na sehemu ambazo mashabiki wanapaswa kukaa kuhakikisha kuwa yana usalama na hayaingiliani na eneo la uwanja kwa usalama - pia ule wa wachezaji na waamuzi.

Kamati ya Leseni za Klabu ndiyo yenye kutembelea na kukagua viwanja hivyo, lakini inasikitisha kuona kwamba viwanja vimeruhusiwa kutumika ingawa mechi moja tu imechezwa na uwanja unaonekana kuwa haufai, hivyo awali hawakugundua upungufu huo na kuruhusu kutumika?

Mbali na eneo la kuchezea mechi, hivi kamati haikugundua upungufu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, maana eneo la kuchezea wanaweza kutafuta sababu kuwa pengine kishindo ama mvua zimenyeesha na kuharibu uwanja.

Lakini vyumbani, sidhani kama katika hali ya kawaida mkaguzi anaweza kushindwa kugundua kwamba vyumba vina shida, virekebishwe kabla ligi haijaanza, maana kama ni uwanja huo wa Karume hata msimu uliopita ulitumika na timu hiyo kama uwanja wa nyumbani.

Ina maana upungufu huo upo kwa miaka miwili tangu Biashara United ipande daraja, misimu yote hiyo hakukuwa na tatizo hilo? Sawa, inawezekana limeonekana sasa, je wakati wa ukaguzi hawakuhisi kitu kama hicho ili wawaeleze mapema wahusika wakirekebishe?

Naamini huko tunakoelekea viwanja vingi vitakuwa vinafungiwa, maana baadhi ya viwanja vilivyopo mikoani sio salama hasa pale mvua zinaponyeesha sehemu ya kuchezea ndio huharibika zaidi.

Kuna haja ya TFF, TPLB kuchukua hatua zaidi kwa hawa wakaguzi wa viwanja hasa ambapo baadaye wanagundua hata vyumba vya kubadilishia nguo vina upungufu wakati eneo kama hilo linaonekana mapema kabla hata wachezaji hawajaingia kubadilisha nguo.

Naamini mabosi wao wanapaswa kuchukua hatua kabla ya kufungia uwanja husika kutumia. Ni vyema kama ikibainika mapema viwanja hivyo viwachukuliwe hatua, lakini iwapo uudhaifu haukuonwa na wajumbe, Bodi inanze na wakaguzi wake kuruhusu viwanja kuanza kutumika wakati vinahitaji marekebisho zaidi.

Sidhani kama ukaguzi unafanywa mara moja, lakini naamini wakaguzi hao wanapokwenda na kugundua matatizo, basi watatoa maelekezo ya kufanya kabla ya kuwaruhusu wahusika kuutumia ambapo wanapaswa kwenda tena kujiridhisha kama yale yaliyopaswa kufanyika - yamefanywa.

Ikiwa tofauti na hivyo, basi wana wajibu wa kuwaeleza kwamba uwanja hautaanza kutumika mpaka masuala huika yashughulikiwe.

Sidhani kama ingefika ilivyo ambapo sasa timu husika za viwanja zitaingia gharama nyingine za kushiriki michezo.

Wanaposafiri watahitaji huduma kama usafiri, malazi na chakula lakini wangekuwa wanatumia viwanja vya nyumbani gharama zingepungua. Hivyo basi TFF, TPLB waaangalie kamati inapokwenda kukagua viwanja huwa inakagua nini.