VIDEO: TFF: Marufuku Manji kurudishwa Yanga kwa mlango wa nyuma

Muktasari:

Yanga inatakiwa kufanya uchaguzi wake Januari 13, 2019 kuziba nafasi ya mwenyekiti na wajumbe wengine waliojiuzuru katika uongozi wa klabu hiyo

Dar es Salaam. Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Malangwe Mchungahela amewataka Yanga kuacha mpango wao wa kutaka kumrudisha mwenyekiti Yusuf Manji kwa mlango wa nyuma kesho, Jumapili.

Akizungumza na wanahabari mwenyekiti Mchungahela alisema wamepata taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa Yanga kesho Jumapili wanataka kuitisha kikao chao cha kumtambua Manji kuwa mwenyeki wao.

“Nataka kuwaonya wasithubutu kufanya kitu cha namna hiyo na watakapofanya hatutawachekea, tutawashughulikia wote.”

Mchungahela alisema mchakato umeshatangazwa nafasi ya mwenyekiti ipo wazi na yeyote anayetaka uwenyekiti asipite mlango wa uwani aje kuchukua fomu si kinyume na hapo vinginevyo hatutakubali.

“Mtu yeyote ambaye ni kiongozi wa mpira mwenye madaraka ya namna yoyote akifanya kinyume cha hapo atashughulikiwa, na taratibu za kimpira ikiwemo kupelekekwa kwenye kamati ya maadili hatutasita na wala tusilaumiane huku baadaye,” alisema Mchungahela.

Awali Mwenyekiti Mchungahela alisema uchaguzi wa klabu ya Yanga ulishaanza tangu ulipotangazwa tarehe 5 na fomu zilikuwa zianze kuchukuliwa kuanzia tarehe 8 -13, lakini ilishindikana kutokana na kuwa na kikao na wajumbe wa kamati ya utendaji wa Yanga.

“Fomu zimeanza kutoka 9 hadi 14 na uchaguzi utakuwa katika tarehe ile ile iliyopangwa,” alisema mwenyekiti huyo..