TETESI MAJUU: Madrid wakimkosa Hazard wanaenda kwa Salah

Muktasari:

  • Inadaiwa kuwa Rais wa Real Madrid, Florentino Perez anajiandaa kulipa kiasi cha pauni 128 milioni kwa Salah ambaye kwa msimu wa pili mfululizo ameendelea kung’ara katika Ligi Kuu ya England na soka la Ulaya kwa ujumla.

REAL Madrid wanafikiria kumnasa staa wa Liverpool, Mohamed Salah kama watashindwa kumnasa nyota wa Chelsea, Eden Hazard ambaye timu yake inaweza isimuuze baada ya kufungiwa kununua wachezaji kwa miaka miwili.

Madrid bado wanateseka na pengo la staa wao wa zamani, Cristiano Ronaldo aliyeuzwa kwenda Juventus katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto na wamepania kununua staa mkubwa wa kuziba pengo lake mwishoni mwa msimu huu.

Inadaiwa kuwa Rais wa Real Madrid, Florentino Perez anajiandaa kulipa kiasi cha pauni 128 milioni kwa Salah ambaye kwa msimu wa pili mfululizo ameendelea kung’ara katika Ligi Kuu ya England na soka la Ulaya kwa ujumla.

Julian Brandt

REAL Madrid na wapinzani wao Atletico Madrid wanavutiwa na mpango wa kumchukua mshambuliaji mahiri wa Bayer Leverkusen, Julian Brandt, ambaye msimu huu amefunga mabao manne na kupika mabao 10 katika mechi 25 za Bundesliga.

Brandts ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza kwa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Low katika michuano ya kombe la dunia mwaka jana nchini Russia huku akisababisha staa wa Manchester City, Leroy Sane asiitwe kikosini.

Antoine Griezmann

INDAIWA kwamba staa wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann anajuatia uamuzi wake wa kukataa dili la kwenda Barcelona katika dirisha kubwa lililopita mwaka jana na sasa anavutika na uhamisho wa kwenda Nou Camp.

Inadaiwa kwamba staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa amejiweka sokoni kwa klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya baada ya Atletico kuendelea kuvurunda msimu huu lakini Barcelona hawana mpango tena wa kumchukua.

Jota

MASKAUTI wa Tottenham wamefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na staa wa Benfica, Jota, 19 wakati wa pambano la michuano ya Europa dhidi ya Dinamo Zagreb ugenini na wamepanga kutoa dau katika dirisha kubwa lijalo.

Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino amekuwa akimfukuzia staa huyo kwa muda mrefu wakati huu Tottenham wakijipanga kutumia pesa kwa mara ya kwanza baada ya madirisha mawili kupita bila ya kufanya hivyo Jota ni miongoni mwa mastaa wanaofukuziwa.

Christian Eriksen

KIUNGO mchezeshaji wa Tottenham, Christian Eriksen ambaye mkataba wake na klabu hiyo unatazamiwa kumalizika katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2020 bado anawindwa na Real Madrid ambayo ameipania kuichezea tangu akiwa mtoto.

Spurs wanaweza kulazimika kumuuza staa huyo katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto kama hatasaini mkataba mpya klabuni hapo na klabu pekee ambayo mpaka sasa inapigiwa chapuo kumnasa ni Real Madrid.

Antonio Valencia

KLABU za West Ham na Inter Milan zinaungana na Arsenal katika mpango wa kumnasa mlinzi wa kulia wa Manchester United, Antonio Valencia wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Baba wa staa huyo wa kimataifa wa Ecuador mwenye umri wa miaka 33 ambaye ni pia ni wakala wake amefichua siri hiyo hivi karibuni na kuna uwezekano mkubwa Valencia akabakia katika soka la Kiingereza msimu ujao

Mauro Icardi

INTER Milan wameiambia Real Madrid kwamba wanataka kiasi cha Euro 80 milioni kwa ajli ya kumruhusu staa wao wa kimataifa wa Argentina, Mauro Icardi kuondoka klabuni hapo na kutua Real Madrid mwishoni mwa msimu.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 hajaichezea Inter Milan tangu alipovuliwa unahodha mwezi uliopita na amekuwa pia akitakiwa na klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya zikiwemo Juventus, Chelsea na Manchester United.

 Francisco Reis Ferreira

LIVERPOOL imefanya mawasiliano na Benfica wakijaribu kuangalia uwezekano wa kumnasa mlinzi mahiri wa nguvu wa Benfica, Francisco Reis Ferreira, 21 mwenye urefu wa futi 6’3 wakati huu wakitafuta patna wa kucheza na Virgil van Dijik.

Ferreira anayejulikana kwa jina la Ferro anatajwa kuwa mmoja kati ya walinzi bora makinda katika soka la Ureno kwa sasa huku Liverpool wakiwa wamemtupia jicho la muda mrefu na kuna uwezekano wakatoa dau kubwa mwishoni mwa msimu.