TAKWIMU: Gor Mahia vs Yanga, nani atacheka leo?

Wednesday July 18 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Leo ndio leo mwanangu, wale wakali wa soka Afrika mashariki wanavaana leo kuanzia saa moja jioni ugani kasarani. Nazungumzia mtanange wa kukata na shoka kati ya mabingwa wa soka wa Kenya, Gor Mahia dhidi ya wababe wa soka kutoka Tanzania, Yanga SC.
Mabingwa hao wanakutana katika mchezo wa tatu wa kundi D, Kombe la shirikisho la Afrika. Kogalo ya Muingereza Dylan Kerr, wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na pointi mbili tu huku Yanga ya Mzambia Noel Mwandila, iliyosafiri kutoka Dar es Salaam, wakijitupa Kasarani wakiwa na pointi moja tu.
Mafahali hawa wanaojivunia rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi za nchi mara 41, Yanga wakibeba VPL mara 27 huku wakibeba KPL mara 16, wanaingia katika mchezo huu, wakihitaji ushindi wa lazima ili kujisafishia njia ya kutinga hatua ya robo fainali. Patachimbika pale Kasarani aisee!
Baada ya kuanza ligi kwa kasi ya ajabu ambapo hivi sasa wanaongoza jedwali wakiwa na pointi 49 na mechi mbili mkononi, wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja, Kogalo wanaonekana kuwa katika katika nafasi nzuri ya kucheka leo, pamoja na kuonekana kuchoka kutokana na mrundikano wa mechi.
Vijana wa Dylan Kerr, wameingia dimbani mara 11 ndani ya mwezi mmoja uliopita, hali ambayo inaweza kuwabeba Yanga jioni ya leo, hasa ukizingatia kuwa Kogalo, hawajapata muda mzuri wa kupumzika na kufanya mazoezi.
Kwa upande wa Yanga, wao hawana sababu ya kufungwa kwani wako fiti kisaikolojia na kimazoezi. Ikumbukwe kuwa Yanga walijitoa kwenye michuano ya Kombe la Kagame, yaliyomalizika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam ambapo walimaliza katika nafasi ya tatu.
Safu ya ulinzi ya Kogalo inayoongozwa na nahodha Harun Shakava inaonekana kutokuwa vizuri na ushahidi ni mechi ya hivi karibuni ya Cecafa dhidi ya Rayon Sports ambapo lucha ya kuongoza 2-0, walijikuta wakifanya uzembe mara mbili na kuruhusu Rayon kusawazisha. Hali hii ilijirudia katika mchezo dhidi ya LLB Academic ya Burundi.

 
Mbali na ubovu wa safu ya ulinzi katika siku za hivi karibuni, kambi ya Kogalo inaonekana kutokuwa na utulivu ambapo taarifa zinaeleza kuwa wachezaji wako katika mgomo baridi wakidai malipo ya posho. Hii ilithibitika walipokataa kupanda jukwaani kuvaa medali za mshindi wa tatu kwenye Kombe la Kagame.
Kitu kingine kinachowabeba Yanga ni kuondoka kwa Straika wa Kogalo, Mnyarwanda Meddie Kagere aliyejiunga na Simba huku tetesi pia zikidai kuwa kiungo kisheti, Francis Nyambura Kahata naye yupo mbioni kuondoka, taarifa zikisema anaenda Simba. Kwa hali hii wazee wa Jangwani washindwe tu wenyewe aisee.
Hata hivyo, Yanga wasifikirie kazi itakuwa rahisi kihivyo maana takwimu zinazungumza. Ni kwamba, kabla ya kufungwa na Azam, takwimu zinaonesha kuwa, Gor Mahia walipoteza mchezo mara moja tu. Walifungwa 2-1 na Polokwane ya Afrika Kusini (Aprili 18).
Kilichotokea baada ya hapo ni kwamba Kogalo walicheza mechi 22 bila kupoteza hata mmoja. Sio kama nawatisha Yanga ila wajiandae kisaikolojia, kwani katika mechi hizo tatu walizopoteza hakuna hata moja waliochezea nyumbani. Gor hawajapoteza katika ardhi ya nyumbani msimu huu.
Tulia kwanza, vijana wa Kerr wamekuwa mzigoni kwa siku 80 bila kuchoka sawa na mechi 22, sawa na mechi moja kila baada tatu. Hapo ndipo ugumu wa mtanange wa leo ulipo. Katika siku hizo 80, wamefanya safari kati ya Kenya, South Africa, Rwanda na Tanzania, tunaelewana?
Kambi ya Yanga nayo haiki salama kivile. Wanaingia katika mchezo huu, wakiwa wananashika mkia kwenye msimamo wa Kundi D, hawajapata ushindi hata mmoja, walifungwa na USM Algiers, wachezaji wao kukosa utulivu na uchungu wa kupoteza ubingwa wao wa VPL kwa watani wao Simba.
Tangu mwezi wa nne, Yanga wamejikuta wakipoteza mechi nane kati mechi 12, ukiwemo mchezo wa kwanza wa kundi D, walipochpwa 4-0 na USM Algiers nchini Algeria bila kusahau matokeo mabovu ya Kombe la Sportpesa Super Cup.
Mara ya mwisho walikutana Julai 18, mwaka 2015, Kombe la Kagame, Gor Mahia wakaibuka washindi, kwa kuitandika Yanga 2-1, Jijini Dar es Salaam. Unakumbuka mwaka 1976? Wakikutana kwa mara ya kwanza, Gor Mahia (Luo Union), walishinda 2-1. Swali ni je, nani atacheka leo?

Advertisement