TAFCA, Afcon imewaachia kitu cha kujifunza ?

Muktasari:

Takwimu hizi zinaungwa mkono na kauli ya Kocha wa Senegal, Aliou Cisse, ambaye alisema alihangaika sana kuishawishi serikali kuwaamini wazawa, hususan yeye na kweli, Matunda yameonekana.

MICHUANO ya 32 ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, imemalizika Ijumaa iliyopita kwa Algeria kukata kiu cha miaka 29 kwa kutwaa ubingwa.

Wapinzani wao kwenye fainali walikuwa Senegal ambao wanaendelea kusubiri wakati wao ufike nao watwae ubingwa.

Tanzania imeshiriki kwa mara ya pili baada ya miaka 39 na bila shaka TFF itakuwa imejifunza kitu kutokana na michuano hiyo.

Lakini kabla ya kuizungumzia TFF, ningependa kuwauliza ndugu zangu wa Chama cha Makocha wa Soka nchini(TAFCA), ‘wamejifunza nini kwenye Afcon?’

Fainali hizo za Misri zilikuwa na timu 24, ikiwa na maana kwamba kulikuwa na makocha 24; wageni 14 na wazawa 10.

Timu 16 zilifuzu kwa hatua ya 16 Bora ikiwa na maana makocha 16 walifuzu kwa hatua hii. Kati yao, tisa walikuwa wageni na saba wazawa.

Timu nane ziliingia robo fainali, ikiwa na maana kwamba makocha nane walitakiwa kuzifikisha timu zao hatua hii. Kati yao, wanne walikuwa wazawa na wanne wageni.

Timu nne zikaingia nusu fainali, ikiwa na maana kwamba makocha wanne waliziongoza timu zao kufikia hatua hiyo. Kati yao, wawili ni wazawa na wawili wageni.

Timu mbili zikafuzu kwa nusu fainali, ikiwa na maana kwamba makocha wawili walifikia hatua hiyo na wote walikuwa wazawa.

Kwa kifupi ni kwamba, timu zilizofanyika zaidi kwenye Afcon hii ni zile zilizokuwa na makocha wazawa.

Takwimu hizi zinaungwa mkono na kauli ya Kocha wa Senegal, Aliou Cisse, ambaye alisema alihangaika sana kuishawishi serikali kuwaamini wazawa, hususan yeye na kweli, Matunda yameonekana.

Somo ambalo nataka TAFCA wajifunze ni la kuendeleza makocha wazawa.

Wakati wenzetu wanapiga hatua kwenda mbele, sisi tunapiga hatua kurudi nyuma.

Wakati Misri wanamfukuza kazi Javier Aguire na kumrudisha mzawa Hassan Shehata, sisi tunamfukuza kazi mgeni Amunike na kumleta mgeni wa muda, Etienne Ndayiragije kutoka Burundi.Burundi?

Ndio, ni Burundi, nchi iliyotoa makocha wengi kwenye Ligi Kuu ya Tanzania hivi karibuni.

Nchi ambayo ilifuzu Afcon 2019 na kucheza mpira mzuri, ikiwa na kocha mzawa. Kitendo cha TFF kuajiri kocha wa muda kutoka Burundi ni aibu kwa TAFCA.

Mwezi Juni mwaka jana, niliandika kuhusu ‘kifafa’ cha TAFCA na kusababisha makocha wazawa kukosa ubora, nikagusia hadi asili ya kuanzishwa kwake.

Wakati huo kocha wa Stars alikuwa mzawa Salum Mayanga, siku chache baadaye akaja Amunike na sasa ndio huyu Ndayiragije.

TAFCA oneni aibu. Hii ni fedheha kwenu. Ukiwa mlinzi halafu mali unazolinda zikipotea wewe nd’o wa kulaumiwa. TAFCA nyinyi ndio walinzi wa taaluma ya ukocha hapa nchini, mali zinapotea lakini nyinyi wala hamshituki, kweli?

Alfred Kidao, wewe ndiye mwenyekiti wa chama hicho, hebu angalia namna ya kuachia hiyo nafasi aje mtu anayeweza kuisogeza mbele TAFCA.

Kufeli kwa TAFCA ndio kufeli kwa taaluma ya ukocha hapa nchini na ndiyo kufeli kwa mpira wenyewe.

Ni jukumu lenu TAFCA kuhakikisha tunakuwa na makocha wengi wazawa wanaoweza kuwaendeleza vijana wetu katika mitaa yote nchini hadi timu ya taifa.

TAFCA kisiwe chama cha kusubiri michango tu, kiangalie namna ya kuyaishi malengo ya kuanzishwa kwake na marehemu Bert Trauttman!