Swahiba wa Samatta ananukia Man City

Manchester, England. UNAMKUMBUKA Leon Bailey? Ndio huyo huyo aliyekipiga na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta pale Genk kabla ya kutimkia zake Bayer Leverkusen ya Bundesliga.
Sasa winga huyo ambaye alisumbua sana akicheza sambamba na Samatta, ambaye naye ametua zake akikipiga na Aston Villa, yuko kwenye rada za Kocha Pep Guardiola pale Manchester City.
Guardiola amewataka mabosi zake kwenda kulipa pauni 40 milioni ili kumnasa winga huyo kwenda kukipiga kwa wababe hao wa Etihad. Kwa sasa Guardiola anajiandaa kumpoteza winga wake, Leroy Sane na anamuona Bailey kama mtu sahihi wa kwenda kuziba pengo hilo kama Mjerumani huyo atatimkia zake Bayern Munich.
Kwa muda mrefu sasa, maskauti wa Man City, wamekuwa wakimfuatilia Bailey (22) na sasa wapo tayari kumaliza dili hilo kama Sane atalazimisha uhamisho wake kutua Allianz Arena.
Kwa mujibu wa Guardiola, Bailey ana uwezo wa kucheza winga zote za kushoto na kulia kama ilivyo kwa Raheem Sterling, ambaye wakicheza pamoja wataifanya Man City kuwa na makali.
Hata hivyo, Man City watalazimika kuchuana na Arsenal ambao nayo imekuwa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya winga huyo wa kimataifa wa Jamaica, ambaye thamani yake ni pauni 40 milioni.