Sven kuzindua kadi Simba

KOCHA mpya wa Simba, Mbelgiji Sven Vanderbroeck pamoja na wachezaji wa timu hiyo watakuwepo kesho Jumamosi katika hafla ya uzinduzi wa kadi mpya za mashabiki ambazo zitakuwa zikisimamiwa na benki ya Equity.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa kadi za wanachama wa klabu ya Simba itaanza saa 2 asubuhi kwenye viwanja vya Sabasaba Mbagala, jijini Dar es Salaam .
Kupitia mtandao wa kijamii wa 'Instagram' ya klabu hiyo wamewakaribisha mashabiki wote kwenye tukio hilo muhimu ambalo mbali ya kuanza kufanyika hapo ila litaendelea nchi nzima ili kila shabiki kuweza kufikiwa karibu na huduma hiyo.
Klabu hiyo iliingia mkataba na benki ya Equity ambao utawezesha benki hiyo kusimamia mradi wa kadi mpya za wanachama na mashabiki ambazo zitaitwa Simba Card.
Kadi hizo zitatumiwa na wanachama pamoja na mashabiki kuweka akiba ya pesa na kutoa pindi wanapotaka kutumia, pia kulipa ada ya kila mwaka, kununua tiketi za kuingia uwanjani na kupata punguzo la mpaka 10%, kwenye maduka makubwa ambayo yatashirikiana na Simba.
Faida kubwa kwa klabu katika kadi hizo ni makato yanayopatikana wakati wa kufungua akaunti, kukusanya ada kisasa mara moja kwa mwaka na kupata takwimu sahihi za mashabiki iwapo kila shabiki atafungua akaunti.