Sven acharuka Msimbazi

Muktasari:

Sven alisema kikosi chake kimebadilika kwa michezo ya hivi karibuni na anatamani kuona spidi hiyo ikiendelea katika michezo yao ijayo na kuwasisitiza vijana wasibweteke kwani kazi bado mbichi.

LICHA ya ushindi wa bao 1-0 iliopata dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Mkuu wa timu wa Simba, Sven Vanderbroeck amewacharukia nyota wake akidai kwa namna walivyocheza wala hawakustahili kushinda kiduchu mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba iliifunga Kagera kwa mara ya pili msimu huu baada ya mkwaju wa penalti wa Meddie Kagere kutinga wavuni kwenye kipindi cha pili na kuwafanya wafikishe alama 59 baada ya mechi 23, lakini Sven alisema kikosi chake kilishambulia sana lango la wapinzani wao ila hawakuzitumia nafasi zao vizuri kupata ushindi.

“Tulitakiwa tumalize mchezo katika kipindi cha kwanza tu, lakini tulishindwa kufanya hivyo na tukawa kama tumejiadhibu wenyewe ndani ya dakika 90 kwa kushinda 1-0 kwa sababu tulikuwa na nafasi kubwa ya kumaliza mchezo,” alisema.

Sven alisema kikosi chake kimebadilika kwa michezo ya hivi karibuni na anatamani kuona spidi hiyo ikiendelea katika michezo yao ijayo na kuwasisitiza vijana wasibweteke kwani kazi bado mbichi.

“Tulistahili ushindi, lakini sio wa bao moja tena la penalti, kwani timu nzima ilicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi, nawapongeza wachezaji lakini wanatakiwa waendelee hivihivi na kuongeza nguvu zaidi kwa mechi zijazo kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa,” alisema Sven.

Tangu walipofungwa na JKT Tanzania bao 1-0, Simba wamecheza mechi tatu mfululizo wakishinda tena bila kuruhusu wavu wao kuguswa kwani waliinyoa Mtibwa Sugar mabao 3-0, Lipuli FC (1-0) na juzi tena wakaicharaza Kagera Sugar kwa bao 1-0 na wikiendi hii wanatarajia kuikaribisha Biashara United Uwanja wa Taifa.

Kwa upande wa Kocha wa Kagera, Mecky Maxime aliwapongeza wachezaji wake kwa kuweza kujitahidi kutoruhusu mabao mengi.

“Leo (juzi) hatujacheza vizuri kabisa na hatujaweza kabisa kumiliki mpira dhidi ya Simba, hivyo nilijua tunafungwa mengi lakini wachezaji wangu wamejitahidi na kupoteza kwa bao 1-0,” alisema.

NYONI ATOBOA SIRI

Beki Erasto Nyoni wa Simba alifichua siri ya morali kuongezeka katika kikosi chao imetokana na wachezaji wote kuwa na msimamo wa kutaka ubingwa msimu huu.

“Kiukweli wachezaji wote tunalitaka kombe na ndio maana tunajituma, tunaendelea kupambana na tunapeana moyo na ukweli ligi ni nzuri, lakini tunatakiwa tuongeze umakini kuweza kufanya vizuri tena,” alisema.