Sven: Ushindi wa Mtibwa Sugar umeshusha presha Simba SC

Muktasari:

Sven tangu amejiunga na Simba amepoteza mechi moja tu ya ligi dhidi ya JKT Tanzania.

Dar es Salaam.Kocha wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenrbroek amesema ushindi wa mabao 3-0 waliopata dhidi ya Mtibwa Sugar yamepunguza presha kwa wachezaji wake.

Sven alisema amekuwa akisikia maneno mengi kutoka kwa mashabiki wa Simba na soka kwa ujumla wakimtaka aondoke katika nafasi hiyo.

"Nimekuwa nikiyasikia maneno na hata muda mwingine kuona lakini haya yote yalikuwa yanatokeo kutokana na mashabiki hao kuona timu yao unafanya vizuri katika mechi za ligi na mashindano mengine," alisema.

"Kwa maana hiyo ushindi ambao tumeupata katika mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa tena ugenini yamepunguza presha katika kikosi chetu haswa kwenye maeneo mengi.

"Presha ya kwanza imeshuka kwa wachezaji ambao baadhi yao walikuwa wakisemwa vibaya na wengine walikuwa wakionekana wanashindwa kucheza vizuri.

"Lakini hata kwetu benchi la ufundi morali hii ya ushindi utakuwa kama chacheu ya kuweza kufanya hivyo katika michezo ijayo.

"Kiukweli unapofundisha timu kubwa kama Simba na kushindwa kupata matokeo mazuri kwa nafasi yangu kama kocha lazima presha itakuwa kubwa, lakini matokeo haya ya ushindi yamepunguza hali hiyo.

"Kikubwa tunakwenda kufanya maandalizi ya kutosha na kwenda kufanya vyema katika mechi ijayo ili kupata natokeo mengine ya furaha kama haya," alisema.

"Mashabiki wa Simba wanatakiwa kufahamu mpira una matokeo matatu ambayo lazima utakutana nayo hata ukiwa na timu bora kiasi gani lakini ligi ni kama marathoni unaweza kuanza taratibu," alisema Sven ambaye tangu amejiunga na Simba amepoteza mechi moja tu ya ligi dhidi ya JKT Tanzania.