Sure Boy huyoo Singida United

Thursday December 7 2017

 

By OLIPA ASSA

KUNA habari za chini chini, kwamba Azam FC walitaka kumpeleka kiungo wao Salum Abubakar ‘Sure Boy’ Lipuli ya Iringa kwa mkopo, lakini amewagomea na kuwaambia wampeleke Singida United.

Chanzo chetu kimesema bado mabosi Azam wana kigugumizi juu ya kumuachia fundi huyo wa mpira, kwani hawajapata mbadala wake huku kiungo mwenzake, Himid Mao,  akiwa njiani kujiunga na Bidvest Wits ya Afrika Kusini, iliyokamilisha usajili naye.

“Kuna mchezaji wanahitaji achukue nafasi ya Sure Boy, lakini bado hawajamalizana naye ndio maana unaona hizo habari bado zipo chini kwa chini,” kilisema chanzo hicho.

Katika hatua nyingine beki wa Stand United ‘Chama la Wana’, Hamad Kibopile, yupo mbioni kujiunga na Majimaji ya Songea, kupitia usajili wa dirisha dogo.

Kibopile aliyewahi kucheza Mbeya City, alisema: “Kazi yangu ni kucheza ikifika wakati kila jambo litakuwa wazi, kwa sasa sisemi chochote.”

Kabopile anayesifika kwa mipira ya kurusha iliyo kama kona, kasisitiza timu nyingi zimemfuata.