Sura za kazi Man United

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo, staa wa PSG, Mbappe aliwatesa mabeki wa Man United, hasa bao la pili, ambalo aliwafanya mabeki wa timu hiyo ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer kuonekana kuwa si kitu.

MANCHESTER, ENGLAND . UMEWAONA Manchester United? Mechi yao ya juzi Jumanne usiku kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya walionyeshwa mpira unavyochezwa walivyokumbana na Paris Saint-Germain.

Kwenye mechi hiyo, Man United ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford, ilichapwa 2-0. Angel Di Maria alipika mabao yote mawili, ambapo moja lilifungwa na Kylian Mbappe.

Baada ya mechi hiyo, kiraka wa zamani wa wababe hao wa Old Trafford, Phil Neville alisema, alivyotazama timu hizo zinavyocheza, kuna wachezaji wawili tu wa Man United ndio wenye uwezo wa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha PSG, akiwataja kipa David De Gea na kiungo Paul Pogba.

Pogba mwenyewe aliyemtaja Neville kwenye mechi hiyo amecheza hovyo na kuonyeshwa kadi nyekundu inayomfanya akose mechi ya marudiano itakayopigwa Paris wiki mbili zijazo.

Katika mechi hiyo, staa wa PSG, Mbappe aliwatesa mabeki wa Man United, hasa bao la pili, ambalo aliwafanya mabeki wa timu hiyo ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer kuonekana kuwa si kitu. Mbappe alikimbia kupita katikati yao na kufunga bao na hapo ikaonyesha wazi, Man United ina ulazima mkubwa wa kusajili beki mwingine wa kati mwenye kiwango cha dunia.

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger alizungumzia beki ya Man United na kusema Jose Mourinho alikuwa sahihi wakati alipokuwa akilalamika timu hiyo haina mabeki wa maana na hilo lilionekana wazi kwenye mechi hiyo ambayo imewafanya Man United kuweka rekodi ya kupoteza kwa mara ya kwanza zaidi ya mabao mawili ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani katika mikikimikiki hiyo ya Ulaya.

Rekodi pia zinaonyesha hakuna timu iliyowahi kugeuza matokeo ya kufungwa mabao mawili na kuendelea ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kisha ikaenda kupindua ugenini na kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutokana na hilo, bila ya shaka ili Man United kutamba tena kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya itahitaji kuwa na huduma ya wachezaji bora kabisa uwanjani, akiwamo Kalidou Koulibaly wa Napoli. Wababe hao kwa siku za karibuni wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kunasa mastaa kibao akiwamo Adrien Rabiot wa PSG, Paul Dybala wa Juventus, Philippe Coutinho wa Barcelona na Gareth Bale wa Real Madrid.