Suluhu ya Lyon yamkera kocha wa Mbao FC

Muktasari:

  • Akizungumza baada ya mchezo huo, Stam alisema viungo wake walishindwa kufanya kile alichowaelekeza na kusababisha kuambulia pointi moja tofauti na matarajio yake.

Mwanza.KOCHA wa Mbao Amri Said ‘Stam’ juzi alishindwa kujizuia kuwabwatukia nyota wake kwa kushindwa kupata pointi tatu dhidi ya African Lyon kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliomalizika kwa suluhu .

Timu hiyo ya jijini hapa ilianza kwa kasi Ligi hiyo, kwa sasa haijapata ushindi tangu mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar, Oktoba 21 ambapo michezo iliyofuata imeambulia sare na vichapo tu.

Juzi Jumanne ikicheza katika Dimba la Kirumba Mwanza ilishindwa kuutumia vyema kwa kuambulia suluhu jambo ambalo lilimkera Kocha huyo na kuwajia juu nyota wake haswa Viungo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Stam alisema viungo wake walishindwa kufanya kile alichowaelekeza na kusababisha kuambulia pointi moja tofauti na matarajio yake.

Alisema kutokana na hali hiyo atahakikisha anafanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza ili mechi inayofuata waweze kupata ushindi na kujiweka zaidi katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

“Ni kweli mashabiki wetu wengi na sisi kwa ujumla tuliamini kupata matokeo mazuri, lakini sijafurahi kwa kilichotokea, lakini viungo wangu ndio wali niangusha, nitahakikisha mapungufu yote tunayafanyia kazi.