Sturridge atua zake Uturuki kupiga mzigo

Muktasari:

Sturridge, ambaye alicheza kwenye vikosi matata kabisa kwenye Ligi Kuu England kama vile Manchester City, Chelsea na Bolton, alikumbana na adhabu ya kufungiwa wiki mbili baada ya kukutwa na hatia ya kubeti.

LONDON, ENGLAND. STRAIKA, Daniel Sturridge ametua kwenye kikosi cha Trabzonspor na kusaini mkataba wa miaka mitatu kukipiga huko Uturuki.

Fowadi huyo wa zamani wa England ametimkia zake Uturuki baada ya kuachwa na Liverpool baada ya mkataba wake kufika mwisho akitamba Anfield kwa kipindi cha miaka sita.

Sturridge alihusishwa na timu nyingi sana kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ikiwamo Marseille, DC United na Aston Villa, lakini mwenyewe ameamua kutimkia huko Uturuki kusaini kuichezea Trabzonspor.

Sturridge, ambaye alicheza kwenye vikosi matata kabisa kwenye Ligi Kuu England kama vile Manchester City, Chelsea na Bolton, alikumbana na adhabu ya kufungiwa wiki mbili baada ya kukutwa na hatia ya kubeti.

Sturridge alicheza mechi 160 kwenye kipindi chake cha miaka sita katika kikosi cha Liverpool na alikuwa sehemu ya kikosi kilichokaribia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2014 na mwaka huu 2019. Shida kubwa iliyokuwa ikimsumbua staa huyo ni majeruhi ya mara kwa mara. Januari mwaka jana alikwenda kwa mkopo West Brom, lakini aliishia kucheza mechi sita tu kutokana na kuwa mgonjwa.

Huko kwenye kikosi kipya Sturridge atakutana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Chelsea, John Obi Mikel.