Straika tishio Kagera Sugar kuwakosa Yanga

Muktasari:

Mhilu anashika nafasi ya pili katika chati ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu akiwa na mabao 13 huku kinara akiwa ni Meddie Kagere mwenye mabao 19

Mshambuliaji nyota wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu ataukosa mchezo dhidi ya Yanga kesho Jumatano Julao 8 saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kutokana na majeraha.

Mhilu anayeshika nafasi ya pili kwenye chati ya ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu akiwa na mabao 13, hatocheza mchezo huo kwa sababu ya maumivu ya misuli ya paja aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting.

"Tatizo ni misuli ya paja na nitakuwa nje kwa siku nne. Ina maana mechi ya Yanga sitacheza. Baada ya hapo nitaanza mazoezi kujiandaa na michezo mingine. Matarajio yangu ni kurudi kwa ubora uleule" amesema nyota huyo wa zamani wa Yanga na Ndanda.

Mhilu alisema ana imani kubwa pengo lake litazibwa vyema na wenzake kwani timu hiyo ina kundi kubwa la wachezaji wazuri.

"Timu inawachezaji wengi wanzuri kwahiyo kukosekana kwangu mimi bado itakua ni nafasi nzuri kwa mtu atakayecheza kwa sababu ni mechi kubwa pia wachezaji wengi wanatamani kucheza.

Hivyo sioni kama itaathiri chochote kutokuwepo mimi na ninaimani tutashinda" amesema Mhilu.

Kagera Sugar inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi iliyopita ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Yanga ambapo ilichapwa mabao 2-1.

Hata hivyo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 3-0