Straika mpya Yanga ataka mabao 30

Muktasari:

Waziri Junior amesajiliwa na Yanga akitokea Mbao ya Mwanza ambayo licha ya timu yake kushuka daraja alikuwa ndio mfungaji bora wa timu hiyo.

Wakati kikosi cha Yanga kikianza mazoezi jana kuelekea msimu mpya mshambuliaji mpya mzawa wa timu hiyo Waziri Junior amesema malengo yake ni kuifungia mabao 30 timu hiyo.

Junior amesema baada ya kuwa mfungaji bora katika timu yake ya Mbao sasa anataka mafanikio zaidi akiwa na Yanga.

Msimu uliopita akiwa Mbao Junior ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Mbao alifanikiwa kuifungia mabao 13.

"Nimejiwekea malengo hayo,naona hapa Yanga kuna nafasi ya kunifanikishia malengo yangu nimepanga kuhakikisha nafunga mabao hayo 30," amesema Junior.

"Unajua Mbao nimefunga mabao 13 na ile ilikuwa timu ambayo haina watu wengi wanaoweza kukutengenezea nafasi hapa Yanga kuna  viungo bora zaidi.

Hata hivyo Junior amesema katika malengo hayo anatambua kwamba changamoto kubwa itakuwa kupigania nafasi ambapo amejipanga kumshawishi vyema kocha wao anayekuja.

"Hapa kocha bado hajafika lakini akifika tu hapo ndio kwa kuanzia nataka kwanza kuhakikisha nafanya vizuri katika kumshawishi kocha ili niwe na nafasi ya kucheza mara kwa mara."