Straika mpya Yanga aichongea Simba

Friday July 19 2019

 

By Thomas Ng'itu

MASHABIKI wa Yanga kwa sasa wanapumua baada ya jembe lao jipya kutoka Namibia kuwahi kambi ya mazoezini mjini Morogoro baada ya awali kuwa na hofu huenda asije kutokana na danadana za ujio wake.

Straika Sadney Urikhob alituliza mzuka wa mashabiki kwa kutua nchini Jumanne na fasta kukimbilia kambini, lakini akafichua kilichomzuia kuwahi mapema Jangwani, akiichongea Simba kwa mashabiki hao na hata wale wa Msimbazi waliovutiwa naye alipokuja kufanya majaribio na kupotezewa.

Urikhob aliliambia Mwanaspoti, akiwa kwao alikuwa akiwasiliana na viongozi wa Yanga, lakini kila lililokuwa linapangwa lilishindwa kutimia na ishu nzima ilikuwa ni Simba waliomleta nchini dirisha dogo la Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

“Kulikuwa na vitu vidogo vilivyonifanya nishindwe kumalizana na Yanga, hasa baada ya kuhisi nimesaini Simba, lakini baadaye walijua ukweli ndio maana leo nipo hapa,” alisema Urikhob aliyepewa jezi namba 17 iliyokuwa ikivaliwa na Amissi Tambwe aliyemaliza mkataba wake Jangwani.

Straika huyo aliongeza, mbali na Simba kumzuia kuwahi kambi, sababu nyingine ni kuwepo kwenye kikosi cha timu yake iliyokuwa ikishiriki michuano ya Nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA). Kuhusu kusaini mkataba wa awali Msimbazi, kipindi alichokuja kufanya majaribio, Urikhob alisema hakukuwa na chochote baina yao.

“Sikusaini mkataba wowote na Simba, sipendi kuliongelea hili kwa sasa, lakini naamini haikuandikwa niwe Simba, ndio maana leo nipo hapa baada ya Yanga kunipa nafasi ya kujiunga nayo, naiheshimu,” alisema.

Advertisement

Urkhob na beki Mghana, Lamine Moro walijaribiwa Msimbazi kwenye dirisha dogo lililopita, lakini Kocha Patrick Aussems hakuwataka na badala yake aliletwa Zana Coulibaly kutokana na hitaji la beki wa kulia.

Ndipo dirisha kubwa, Yanga wanaamua kuwasaini, wakiwa miongoni mwa nyota wapya 13 walioingia kwenye kikosi kipya cha Kocha Mwinyi Zahera kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Rekodi za Urikhob zinaonyesha katika timu kama sita alizopita amefunga jumla ya mabao 56 tangu mwaka 2013.

Ameichezea Amazulu ya Afrika Kusini mechi 20 na kufunga mabao tisa katika msimu mmoja wa 2013-14, Saraburi ya Thailand (2015) mechi 30 mabao 12, 2016-2017 alikuwa Super Power Samut Prakan ya Thailand na kucheza mechi 42 na mabao 15.

Pia, alikipiga Police Tero FC ya Thailand katika mechi 17 akiifungia mabao sita, PSMS Medan ya India aliyoichezea mechi 11 na kufunga bao moja kisha kurudi Tura Magic ya kwao na kuifungia mabao 13.

Advertisement