Straika mpya Simba kumpiku Kagere, Bocco

MABINGWA wa soka nchini Simba wamemalizana na straika wa KMC, Charles Ilanfya ambaye ameonyesha kujiamini mbele ya Meddie Kagere na John Bocco.

Ilanfya ni miongoni mwa nyota wapya waliosajiliwa Simba akiwemo beki wa kulia David Kameta 'Duchu' aliyetokea Lipuli FC ya Iringa.

Ilanfya ambaye amefunga mabao manne msimu uliopita anakwenda kugombea namba na Mfungaji Bora wa ligi Kagere aliyemaliza na mabao 22 pamoja na nahodha wao Bocco.

Akizungumza na Mwanaspoti Online leo Ijumaa Agosti 7, 2020, Ilanfya amesema kila mchezaji anapotua Simba, Yanga ama Azam anakuwa na malengo yake na wengi wao huridhika na mafanikio hivyo wanajikuta wanabweteka.

"Binadamu tunatofautina nimeona kuna wenzangu wamefika Simba wameshindwa kufanya vizuri lakini binafsi naenda kupambana na kuonesha ushindani dhidi ya mastraika nitakaowakuta ili nipate nafasi ya kucheza dhidi yao jambo ambalo naamini linawezekana," amesema.

"Unapofika katika malengo yako ya kucheza timu kubwa za hapa nchini lazima uwe na ratiba tofauti na ile ya awali kwanza ambalo nitalifanya kwangu kuongeza urafiki na viwanja vya mazoezi pamoja na gym ili kuimarika zaidi ya nilivyo wakati huu," amesema

Kwa upande wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesema Simba, msimu ujao wanaiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa hivyo wanapaswa kufikiria zaidi usajili bora.

"Ukimuangalia Ilanfya ambaye Simba inasemekana wamemsajili huyo sidhani kama ni straika sahihi hasa katika mashindano ya kimataifa kwani usajili huo umelenga zaidi mashindano ya ndani ambayo wana wachezaji wenye uwezo wa kucheza waliokuwa ndani ya timu,"

"Simba wanatakiwa kusajili straika mwenye uwezo wa kufunga kweli kwani ukiangalia Ilanfya msimu huu hajafikisha mabao hata robo ambayo amefunga Kagere ambaye anakwenda kushindana naye nafasi moja.

"Dirisha bado halijafungwa wanatakiwa kuweka nguvu na kuangalia sokoni kuna mshambuliaji gani ambaye anaweza kufunga na hata ukimpambanisha na Kagere au Bocco anapata nafasi dhidi yao na huyo ndio wanatakiwa kuwa nae," amesema na kuongeza

"Kuna baadhi ya mastraika ambao wamesajiliwa Simba na kuonekana wameshindwa kufanya vizuri hilo limechangiwa na ubora ambao wameonesha Kagere na Bocco ambao ni ngumu kuwaweka nje na kutoa nafasi kwa wengine,"