Straika Simba alia kukosa pambano la watani

Muktasari:

  • Straika huyo alikipiga Simba kwa msimu wa 2012/13 ambapo aliweza kucheza kwa msimu mmoja kisha kuondoka klabuni hapo na kwenda kusajiliwa na Mtibwa Sugar.

STRAIKA wa zamani wa Simba, Abdallah Juma amesema katika jambo ambalo linamuumiza mpaka sasa ni kushindwa kucheza pambano la watani wa jadi katika kipindi ambacho alicheza Msimbazi.
Simba na Yanga wanatarajia kukutana keshokutwa katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, mchezo utakapigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Juma alikipiga Simba msimu mmoja wa 2012/13 kisha kutimkia Mtibwa Sugar, ameiambia Mwanaspoti Online kuwa ni heshima kubwa kucheza mechi hizo za watani ingawa kwake hakubahatika kucheza .
Amesema msimu aliocheza Simba pambano la kwanza alikuwa na jeraha la kifundo cha mguu hivyo kuukosa mchezo huo huku mechi ya mzunguko wa pili hakupangwa kikosini.
“Hiki kitu kinaniumiza hadi sasa kila likija pambano la hizi timu huwa nakumbuka niliposhindwa kucheza, unajua ni heshima kubwa sana kuwepo kwenye kikosi kwani mechi hii huwa inawakutanisha wababe wa soka hapa nchini,” amesema Juma.
Straika huyo ambaye kwa sasa anakipiga Mashujaa  FC, amesema anaamini bado ana nguvu na kwamba kuna siku ndoto za kucheza pambano hilo zitatimia.
“Bado ninacheza soka hivyo sijakata tamaa kabisa, nina imani kuna siku nitacheza hili pambano kwani nitapambana ili kiwango changu kiwe sawa na kuweza kupata nafasi ya kusajiliwa kwenye hizi timu mbili,” amesema mshambuliaji huyo.