Straika Prisons awagomea Waarabu kisa, acheze Yanga

Thursday December 7 2017

 

By MWANDISHI WETU

MKALI wa mabao wa Prisons, Mohammed Rashid amewagomea Waarabu wa Misri waliomtaka kwenda kufanya majaribio katika klabu moja nchini humo, kisa ikiwa ni kukamilisha usajili wake Yanga inayoonekana kumtaka.

Straika huyo aliyefunga mabao sita mpaka sasa Ligi Kuu Bara, amealikwa kwenda Misri pamoja na nyota wa Njombe Mji, Ditram Nchimbi na kama watafanya vizuri watasajiliwa moja kwa moja nchini humo.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kwamba Rashid anayetajwa kuwa straika hatari zaidi Ligi Kuu, amegoma kwenda nchini humo akitaka kusajiliwa moja kwa moja, kwani tayari mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wameahidi kumpa ulaji ambao hataki kuupoteza.

“Walikuwa waende pamoja na Ditram Nchimbi lakini yeye amegoma, Yanga wameongea naye hivyo anawasikilizia kwanza, naona analenga zaidi kucheza hapa,” alisema mtu wa karibu wa Rashid huku akionyesha kumshangaa kiasi fulani.

“Ditram amekubali na tayari anafuatilia hati ya kusafiria ili aende huko, ameanza kujifua pia ili aweze kwenda kufanya vizuri,” alisema.

Hata hivyo klabu yake ya Prisons imedai kwamba haina taarifa zozote za staa huyo kuhitajika Misri, huku pia ishu yake ya kutua Yanga wakiisikia tu juu kwa juu.

Katibu Mkuu wa Prisons, Havintish Abdallah alisema Yanga hawajapeleka ofa yoyote mezani hivyo kama wanafanya mazungumzo nyuma ya pazia na mchezaji huyo, basi wataumia kwani ana mkataba nao.

“Yanga wakija tutazungumza nao, hatuna shida, kikubwa wafuate taratibu. Tunachofahamu ni kwamba Rashid anatakiwa kuwasili Mbeya kesho (leo) Alhamisi,” alisema Abdallah aliyewahi kuitumikia timu hiyo.

Kuhusu usajili wao alisema; “Tunataka kuongeza straika, kipa pamoja na kiungo, tayari tumeanza mazungumzo na wachezaji hao na wako huru, hivyo tutakamilisha mapema.”