Straika Polisi Tanzania kukomaa na ligi ya Bongo

Muktasari:

 Mdamu aliibukia katika shule ya michezo ya Alliance na hadi sasa ameshacheza katika timu tatu tofauti ambazo ni Alliance, Kariobang Sharks na Polisi Tanzania.

STRAIKA  wa Polisi Tanzania,Atanas Mdamu amesema kwake hatamani tena kucheza soka la kulipwa katika nchi za Afrika Mashariki na ni bora abaki hapa nchini ambako wanalipa vizuri .

Mshambuliaji  huyo msimu uliopita alichezea Kariobang Sharks inayoshiri ligi kuu ya Kenya kwa miezi sita akitokea Singida United kisha msimu huu kurejea nyumbani katika timu ya  Alliance ingawa mzunguko wa pili alijiunga na Polisi Tanzania.

Mpaka sasa Winga huyo ameshacheza mechi Saba za ligi kuu akiwa na kikosi cha Polisi Tanzania ambapo hajafunga bao lolote ingawa amepiga pasi mbili zilizozaa mabao.

 Akizungumza na Mwanaspoti Online,Mdamu(23),alisema amecheza Kenya kwa kipindi cha miezi Sita lakini amegundua soka la Tanzania linalipa  kuliko katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.

“Kule Kenya maisha magumu sana hakuna pesa huku bongo afadhali kidogo unalipwa mishahara na posho kwa wakati sitamani tena kwenda kucheza soka nchi za Afrika Mashariki labda Ulaya au sehemu nyingine ya Afrika.

Ni bora nibakie hapa hapa Bongo kwani unalipwa kwa wakati angalia nipo Polisi Tanzania nalipwa vizuri na maisha yako sio mabaya nimecheza ligi kuu ya Kenya pagumu sana kwanza mashindano yao hayana mvuto sana kama hapa nyumbani,” alisema Mdamu.

Alisema ni bora kubaki kucheza hapa bongo ambapo ligi yake ni bora na timu zinalipa kwa wakati na maisha sio magumu sana kuliko kucheza huko unaambulia sifa ya kucheza nje ya nchi lakini mfukoni unakuwa una kitu.

 Alisema kwa sasa anajipanga kuhakikisha anapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwani alijiunga na timu hiyo kwenye dirisha dogo la usajili akitokea Alliance hivyo anatakiwa kukomaa ili aweze kupata namba kwenye klabu hiyo.

Mdamu alisema katika kikosi hicho pamoja na Mdamu lakini pia wapo  washambuliaji Sixtus Sabilo,Matheo Antony,Henrico Kayombo,Marcel Kaheza jambo ambalo limefanya kuwepo kwa ushindani wa namba.

“Nimesajiliwa hapa kwenye dirisha dogo la usajili hivyo ninatakiwa kukomaa na kuhakikisha napata namba kwenye kikosi cha kwanza kwenye michezo hii iliyobakia ya ligi kuu,” alisema.

Polisi Tanzania hadi sasa wako katika nafasi ya Sita kwenye msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi 45 ambapo wamebakiza mechi tisa kumaliza mashindano hayo msimu huu.