Straika Nchimbi wa Azam FC atua Mwadui FC

Muktasari:

Dirisha la usajili limefunguliwa jana na tayari Mwadui FC imefanikiwa kumnyakuwa kwa mkopo mshambuliaji wa Azam FC, Ditram Nchimbi ili kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Mwanza. Mwadui FC imefanikiwa kumnasa mshambuliaji wa Azam FC, Ditram Nchimbi kwa mkopo wa muda mrefu hadi mwisho wa msimu.

Nyota huyo wa zamani wa Njombe Mji alitua Azam mwanzoni mwa msimu huu, lakini ameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kocha  Mholanzi, Hans Pluijm.

Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Ally Bizimungu aliithibitishia Mwanaspoti kumnasa Straika huyo kwa mkopo ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.

Alisema kuwa kutokana na mipango yao katika kuiweka timu katika nafasi nzuri wameona Nchimbi atasaidia kwa kiasi fulani.

"Tayari tumemnasa Nchimbi kwa mkopo kutoka Azam FC ili kuongeza nguvu katika nafasi ya ushambuliaji kwahiyo tunaamini atasaidia kufikisha malengo yetu" alisema Bizimungu.

Kocha huyo Mnyarwanda aliongeza kuwa mkakati wao ni kuongeza wachezaji wanne akiwamo Nchimbi, ambapo hadi sasa mazungumzo yanaendelea vizuri na nyota wengine ambao kama mambo yatakuwa sawa basi watawatambulisha.

Alisema kuwa nafasi atakazoongezea nguvu ni kwenye sehemu ya ushambuliaji ili kupata mabao na kiungo wa kati ili kuimarisha vizuri timu.