Straika Mwadui ampigia hesabu kali Makambo

Muktasari:

 

 

  • Mwadui inajitupa uwanjani kesho Alhamisi kuwakabili Coastal Union, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Mwadui Complex, ambapo timu zote zilipata ushindi katika mechi zilizopita.

MWANZA. STRAIKA wa Mwadui FC, Salim Aiyee juzi alifikisha bao la kumi msimu huu,huku akimpumulia nyota wa Yanga, Heritier Makambo mwenye mabao 11, lakini kinda huyo amesema kuwa kesho Alhamisi huenda akampita Mkongo huyo katika ufungaji mabao.

Mwadui ambayo imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, itakuwa tena kibaruani kwenye uwanja wao wa nyumbani kuwavaa Coastal Union, mchezo utakaopigwa mkoani Shinyanga.

Hadi sasa Makambo raia wa DR Congo ndiye anaongoza kwa mabao 11, huku Aiyee (Mwadui FC), Eliud Ambokile (Mbeya City) na Said Dilunga wa Ruvu Shooting wakiwa na 10.

Aiyee alisema kuwa kwa sasa kiu yake ni kuongoza katika ufungaji bora na kwamba kutokana na ushirikiano uliopo kikosini uwezekano upo wa kumpita Makambo katika ufungaji mabao na leo kazi ndio inaanza.

Alisema kuwa licha ya kuwania tuzo ya mfungaji bora msimu huu, malengo yake ni kuisaidia timu kupata matokeo mazuri na kujinasua nafasi za mwisho katika msimamo wa Ligi kuu.

“Nitaendelea kupambana kwa sababu natamani kuongoza orodha ya wafungaji, lakini malengo yangu ni kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri ili kukwepa rungu la kushuka daraja,” alisema Aiyee.

Kwa upande wake, kocha wa kikosi hicho Ally Bizimungu alisema kuwa baada ya ushindi katika mchezo uliopita sasa wanahitaji pointi tatu nyingine leo dhidi ya Coastal Union ili kujiweka nafasi nzuri.

Alisema kuwa kikosi chake kipo fiti na hakuna mwenye tatizo lolote hivyo mchezo wa leo watapambana kufa na kupona ili kupata matokeo mazuri kwani wana hasira kutokana na mechi nyingi walizopoteza.

“Timu ipo vizuri na vijana wana ari na morari,kikubwa ni kuhakikisha hatufanyi makosa kwani wapinzani wametoka kupata ushindi mechi ya mwisho ugenini kwahiyo tutakuwa makini nao,” alisema Bizimungu.