Straika Msimbazi apelekwa Yanga

Muktasari:

Dk Msolla alisema lakini straika huyo chipukizi akifanya kazi na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ni rahisi kung’ara kwa vile Mkongomani ana uwezo mkubwa wa kumrejeshea makali yake.

HII inaweza kuwa taarifa nzuri kwa Wanajangwani, baada ya Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla kufichua kuwa, straika wa Simba Adam Salamba hawezi kubadilika mikononi mwa Patrick Aussems.

Dk Msolla alisema lakini straika huyo chipukizi akifanya kazi na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ni rahisi kung’ara kwa vile Mkongomani ana uwezo mkubwa wa kumrejeshea makali yake.

Salamba alisajiliwa Simba akitokea Lipuli FC ya Iringa akiwa ndiye mfungaji bora wa timu hiyo, lakini amekuwa hana msimu mzuri Msimbazi kwani amefunga mabao matatu tu na Msolla alisema kwa Mzungu hataweza kubadilika abadani.

Dk. Msolla alisema timu nyingi nchini hazina wataalamu wa saikolojia wa kusaidia wachezaji jinsi ya kuishi wanapokuwa kwenye majukumu ya timu zao na nje ya kazi hasa kumudu matatizo ya kifamilia.

“Salamba wa Simba sio Salamba yule wa Lipuli, ni mchezaji mdogo lakini amepotea katika soka, baada ya kutua Simba nadhani alisahau majukumu yake mengine, kama hana mambo mengi basi kuna vitu vinamuathiri ambavyo kocha alipaswa kufahamu.

“Kwa timu kubwa hapa nchini kocha pekee anayeweza kukaa na wachezaji na kuwajenga kisaikolojia akiona wanashuka ni Zahera, hata Salamba angekuwa kwake asingefika alipo, nadhani Aussems anaangalia zaidi mafanikio yake huku vipaji vya wachezaji wachanga vikiporomoka.

“Salamba alikuwa ni moja ya wachezaji tegemeo wa timu ya Taifa lakini mwelekeo wake wa sasa unasikitisha na kukatisha tamaa hata huko Ubelgiji akiendelea hivi atafeli, anatakiwa kujengwa zaidi, anapata nafasi ya kucheza hata zaidi ya dakika 20 ila hakuna anachokifanya, hapo ni lazima kuna tatizo na linatakiwa kufanyiwa kazi.