Straika Mbao apata mzuka

Straika wa Mbeya City, Eliud Ambokile

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Said alisema kufanya vizuri kwa Ambokile kama mchezaji kijana ni kitu kikuba ambacho kijana yoyote anatamani kukifanya ili kujiweka sehemu nzuri.

KASI ya ufungaji anayokwenda nayo straika wa Mbeya City, Eliud Ambokile, imemuongezea morali mshambuliaji wa Mbao, Said Said Jr.

Ambokile mpaka hivi sasa ndio kinara wa mabao Ligi Kuu akiwa na mabao 8, huku kwa upande wa Said akiwa na magoli matano wote wakiwa wachezaji ambao, ni msimu wao wa pili katika Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Said alisema kufanya vizuri kwa Ambokile kama mchezaji kijana ni kitu kikuba ambacho kijana yoyote anatamani kukifanya ili kujiweka sehemu nzuri.

“Ambokile ananifanya nijitume zaidi, ana spidi nzuri katika ufungaji kiukweli ananipa changamoto ya kufanya vizuri zaidi yay eye anavyofanya, juhudi za mazoezi naamini nitafanikiwa,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mabao ambayo amepanga kufunga msimu huu licha ya kwamba mpaka hivi sasa amefunga mabao matano, alisema anataka kufunga zaidi. “Nataka kufunga zaidi ili niweze kuisaidia timu yangu, nimepanga nifunge mabao 20 nitajitahidi kufanya hivyo au kufikia nusu yake, kikubwa ni kumuomba Mungu anijaalie afya njema,” alisema.