Straika Kapera amtia presha Kagere, Ambokile

Muktasari:

Mshambuliaji Kapera ameshafunga mabao matatu akiwa ameachwa kwa bao moja na nyota wa Simba, Meddie Kagere huku straika wa Mbeya City,Eliud Ambokile akiongoza kwa ufungaji wa mabao sita katika Ligi Kuu.

Mwanza. Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Ramadhan Kapera amesema mambo yataendelea kumnyookea anaweza kubeba tuzo ya mfungaji bora msimu huu.

Mshambuliaji huyo ni msimu wake wa pili kucheza Ligi Kuu baada ya msimu uliopita kukipiga Majimaji iliyoshuka saraja, ameshafunga mabao matatu na kuisaidia timu yake kupanda hadi nafasi ya 10 kwa pointi 12 baada ya mechi nane.

Kwa idadi hiyo ya mabao Kapera anaingia orodha ya wafungaji wenye mabao mengi akitanguliwa na Straika wa Mbeya City, Eliud Ambokile aliyefunga mabao sita akifuatiwa na Meddie Kagere wa Simba magoli manne.

Kinda huyo alisema kutokana na mwanzo mzuri huenda mwisho wa ligi mambo yakamnyokea na kuweza kutwaa kiatu cha mfungaji bora.

Alisema kuwa mbali na kujituma, lakini ushirikiano wake na wachezaji ndani ya timu pamoja na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi anaamini atafikia malengo yake.

“Kwanza nikumshukuru Mungu kwa kuwa tayari nimefikisha idadi hii ya mabao licha ya kwamba Ligi ni ngumu, lakini nasema lolote linaweza kutokea kwa sababu mbali na kujituma bado nina ushirikiano na wenzangu”alisema Kapera.

Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa kwa sasa anajipanga na mbinu mpya kwani mabeki wa timu pinzani wakishagundua Straika msumbufu huwa wanamkamia hivyo anakuja kivingine.

Alisema kuwa kwa msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza kukipiga Kagera Sugar anahitaji kuacha historia ndani ya timu hiyo ikiwa ni kuisaidia kumaliza katika nafasi nzuri na yeye kuwa mfungaji bora.

“Naendelea kupambana lakini kuwasoma mabeki wa timu pinzani ili kufikia malengo yangu,nataka niache historia hapa Kagera Sugar kwa kuiweka nafasi nzuri lakini nifunge mabao mengi”alisema Straika huyo.