Stevenson : Ngumi jiwe aliyeipa heshima Cuba

Muktasari:

Katika orodha ya wanariadha waliofuata mkondo huu ni pamoja na George Foreman, Muhammad Ali na Joe Frazier. Lakini fedha na ahadi za maisha ya raha hazikumvutia Stevenson na alikataa kuingia katika ngumi za kulipwa licha ya nchi yake kumruhusu.

KILA nchi huwa na mambo yanayoipa umaarufu na watu wa nchi za mbali kujua uwepo kwake.

Kwa mfano watu wengi wameijua Afghanistan na hata miji ya kama Kandahar kutokana na mapigano ya muda mrefu yaliyogharimu maisha ya maelfu. Hivyo hivyo, kwa nchi kama Somalia, Palestina, Sudan au Syria hivi sasa.

Nilishangaa 1974 kusikia watu wa New Zealand, Australia, Carribean, Asia na Arabuni wakisema hawakuijua nchi inayoitwa Tanzania, Mlima Kilimanjaro au Mbuga ya Serengeti hadi mwanariadha Filbert Bayi alipoweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 katika michezo ya Jumuiya ya Madola kule Christchurch, New Zealand.

Mbali ya umaarufu wa kiongozi wa Cuba, mwanamapinduzi Fidel Castro, wapo watu walioijua Cuba baada ya kujitokeza wanariadha walioutikisa ulimwengu na kuvutia watu kila pembe ya dunia.

Miongoni mwao ni mwanandondi ambaye mara tatu alikuwa bingwa wa ngumi za uzito wa juu za Olimpiki na kuwa bingwa katika michezo ya kimataifa ya Amerika ya Kusini, Teofilo Stevenson, aliyefariki 2012, akiwa na miaka 60 baada ya kung’ara miaka ya 1970.

Alishinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki 1972 kule Munich, Ujerumani na nyengine ya michezo hii iliyofanyika Montreal, Canada, miaka minne baadaye. Katika mwaka 1980 alishinda medali ya tatu ya michezo ya Olimpikiiliyofanyika Moscow, Urusi.

Stevenson alisifika kwa uzito wa makonde yake, hasa za mkono wa kulia zilizowapasua uso wapinzani na kuwatoa damu nyingi. Wanandondi waliong’ara katika Olimpiki miaka ya nyuma, walitumia michezo hii kama daraja la kuwa wachezaji wa kulipwa.

Katika orodha ya wanariadha waliofuata mkondo huu ni pamoja na George Foreman, Muhammad Ali na Joe Frazier. Lakini fedha na ahadi za maisha ya raha hazikumvutia Stevenson na alikataa kuingia katika ngumi za kulipwa licha ya nchi yake kumruhusu.

Hii ilitokana na mapenzi na utiifu kwa Cuba na kusema hakuna kiwango cha fedha ambacho angelilipwa kingekuwa na thamani kama nchi yake. Aliwashangaa wanamichezo waliohama Cuba na kwenda uhamishoni kuishi kama wakimbizi au kuchukuwa uraia wa huko.

Stevenson alikataa kibunda cha dola milioni 5 (zaidi ya Sh. 10 bilioni), fedha nyingi katika miaka ya 1970, zilizowekwa mezani kumshawishi awe bondia wa ngumi za kulipwa na apandishwe ulingoni na wanamasumbwi nyota kama Muhammad Ali na Joe Frazier. Alipoulizwa kwa nini alikataa fedha hizo ambazo zingempatia maisha mazuri, Stephenson, kipande cha mtu mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5 alijibu: ”Dola milioni mbili au 10 ni kitu gani ukilinganisha na mapenzi yangu kwa watu wa Cuba?”

Alisema ndondi za kulipwa zinakugeuza kuwa bidhaa inayosubiri kuuzwa na hutupwa kama bidhaa iliyooza pale nguvu za kupigana zikipotea na akaongeza kwamba angelifikiria kuwa bondia wa ngumi za kulipwa akiwa kaburini.

Mwanandondi huyu ni miongoni mwa wanamichezo walioipatia sifa Cuba katika michezo kama Alberto Juantorena, mkimbiaji wa mita 400 na 800 ambaye alijulikana kama “Farasi wa Mapinduzi”.

Juantorena alishinda medali za dhahabu za mbio za mita 400 na 800 katika michezo ya Olimpiki.

Stevenson alizaliwa 1952 katika mji wa Delicias-Puerto Madre, kaskazini mwa Cuba. Baba yake alikuwa mhamiaji kutoka visiwa vya Saint Vincent na mama yake Dolores Lawrence alizaliwa Cuba.

Baba yake alifika Cuba 1923 kutafuta kazi na miongoni kazi yake za awali ilikuwa kufundisha lugha ya Kiingereza. Mzee huyu naye alikuwa na umbo kubwa ambalo alilitumia vizuri katika ndondi, lakini aliacha kutokana na mchezo kujaa rushwa na kuona alitumiwa kunufaisha watu wengine.

Wakati baba yake akipigana, yeye alipotimia miaka 9 alianza kuzikunja ngumi na watoto wenzake. Kabla ya hapo alifanya mazoezi ya ngumi kwa siri kwa kuhofia wazazi wake wangelimkataza.

Alihamia Havana akiwa na miaka 13 ili kupata mafunzo ya ndondi yalitotolewa na mwalimu wa Kirusi. Mama yake hakufurahia na alimwambia atapoumia anapopigana akumbuke alimuonya juu ya hatari ya mchezo wa ndondi.

Katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano chini ya mwalimu John Herrera alishindwa kwa pointi na Luis Enriquez, mpiganaji aliyekuwa na uzoefu mkubwa.

Haikumchukuwa muda akawa bingwa wa mashindano ya vijana chipukizi na bingwa wa mashindano ya vijana wakubwa 1968. Akiwa na miaka 17 alishiriki mashindano ya watu wazima, lakini alishindwa katika fainali na mpiganaji aliyetamba zama zile, Gabriel Garcia.

Tangu kushindwa na Garcia kazi aliyoifanya Stevenson haikuwa ndogo kwani kila aliyepambana naye alijijutia kwa kutolewa nje katika mzunguko wa kwanza hadi wa nne. Kwa namna alivyopigana Cuba ilijenga matumaini ya kushinda medali ya kwanza ya dhahabu katika Olimpiki za 1972, miaka 68 tangu kupata medali ya mwisho kama hiyo 1904.

Miezi michache kabla ya michezo ya Olimpiki ya 1972 iliyofanyika Ujerumani Magharibi, Stevenson akiwa na miaka 20 alipambanishwa na pandikizi la baba Ludwik Denderys wa Poland ambaye alikuwa akitisha kwa kuwatoa kwenye ulingo wapinzani baada ya dakika chache za mchezo.

Lakini Stevenson alihitaji sekunde 30 tu kumchakaza Denderys ambaye baadaye alisema alihisi kama vile alipigwa na radi.

“Huyu mtu ni hatari, mkifanya mchezo ataua na ni vizuri apigwe marufuku au apigane kwa kutumia mkono mmoja,” alisema Denderys.

Katika michezo ya 1976 iliyofanyika Montreal, Canada, Stevenson aliwatoa wapinzani watatu kirahisi.

Baada ya michezo ya Olimpiki iliyofanyika Urusi, mameneja maarufu wa ndondi wa Marekani wa zama zile, Don King na Bob Arum, walimshawishi ajiunge na ngumi za kulipwa kwa kumpa ahadi za kuvutia za fedha, lakini aliwaambia wanaweza kuinunua Cuba lakini sio yeye.

Aliporudi nyumbani alipokewa kama shujaa na serikali ilimpa zawadi ya nyumba mjini Havana, gari mbili na nyumba ya mapumziko ya vyumba vitano kwenye ufukwe wa bahari wa Delicias.

Stevenson alishindwa katika raundi ya kwanza ya mashindano ya ubingwa wa dunia ya 1983 na Francesco Damiani wa Italia na kutoa dalili kuwa akiwa na miaka 31 umri haukumruhusu kupigana.

Hata hivyo, alishinda tena ubingwa wa dunia 1986, akiwa na miaka 34 na baada ya hapo alistaafu.

Mwaka 1999 alikamatwa akijiandaa kupanda ndege katika uwanja wa Miami, Marekani, kwa kumpiga kichwa na kumng’oa meno mawili karani aliyekuwa anaikagua tiketi yake kutokana na kuitukana Cuba. Aliachiwa.