Steve Nyerere apigwa benchi msiba wa Mzee Majuto

Dar es Salaam. Muigizaji Steve Nyerere amekua mstari wa mbele kuwaunganisha wasanii hasa katika kipindi cha misiba au matatizo yanayowatokea wasanii wenzao, amepigwa benchi kwenye msiba wa Mzee Majuto.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuundwa kamati ya kushughulikia msiba huo ambayo imeundwa na Chama cha waigizaji Mkoa wa Kinondoni (TDFAA)pamoja na chama cha waigizaji Taifa.

Mbali na misiba, kamati hiyo itashughurikia maafa, nidhamu, maadili pamoja na kushughulikia mikataba mibovu.

Kuondolewa kwa Steve ni kutokana na kutokuwa mwanachama  wa TDFAA  hivyo hawezi kuteuliwa katika kamati.

Mara baada ya Mzee Majuto kufariki, wajumbe wa kamati walifika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya taratibu za kuhifadhi mwili na wakatoa tamko

 Kwamba taratibu zote za kuaga zitafanyika Muhimbili na baadae kusafirisha kwenda Donge, jijini Tanga kwa maziko.

Wakati hayo yakiendelea Steve Nyerere alifika Muhimbili milango ya saa sita usiku, akija na utaratibu mwingine kuwa shughuli za kuaga zifanyike kwenye viwanja vya Karimjee kwa kuwa Majuto ni mtu maarufu, na tayari walishaanza kukaa kikao na wasanii wenzake kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kuagiwa kwenye viwanja hivyo.

Hata hivyo, alipotoa wazo hilo, mmoja wa wanandugu Ashraf, alimwambia kuwa lazima wawasiliane na wanandugu wengine kwa hatua hiyo.

Pamoja na wazo hilo kukubalika, Nyerere alibaki pembeni na hata alipoulizwa zaidi kuhusu utaratibu alikataa kwa kuwa si mwanakamati wa kamati ya maziko

“Mimi sihusiki na chochote kwani nimekuwa nikitukanwa kwamba nakusanya pesa za rambirambi kisha ‘anazitafuna”.

 Steve amekua akitukanwa na baadhi ya watu na mastaa wenzake kutokana na kuonekana mara nyingi kuwa mstari wa mbele kwenye shughuli mbalimbali hasa za misiba ambapo amesema katika msiba wa Mzee Majuto yeye ni muombolezaji kama waombolezaji wengine hivyo hahusiki na chochote.

Hata hivyo; katibu wa TDFAA, Mathew Bicco aliwahi kusema kuwa Steve hataki kujiunga na chama chao,hivyo hana sifa ya kushiriki katika kamati, na ukizingatia chama hicho ni cha muda mrefu na wasanii mbalimbali wanajiunga.

 Mzee Amri Athumani aliaga dunia jana majira ya saa 2:00 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa.