Stars yapanda nafasi moja viwango vya ubora Fifa

Muktasari:

Pamoja na Uganda kuporomoka nafasi mbili bado imeendelea kuongoza kwa ubora kwa ukanda wa Cecafa ikifuatiwa na Kenya.

Dar es Salaam. Tanzania imepanda kwa nafasi moja katika orodha ya viwango vya ubora wa soka kutoka nafasi 138 hadi 137.

Fifa imetoa orodha ya viwango vya ubora leo Alhamisi Februari 7, 2019, Tanzania imepanda kwa nafasi moja baada ya kupata pointi 1087 kutoka ile ya mwezi uliopita.

Wapinzani wa Tanzania katika kusaka tiketi ya kucheza Afcon 2019, Uganda imeshuka kwa nafasi mbili ikiwa nafasi ya 77, ikiwa na pointi 1320, wakati mwezi uliopita ilikuwa 75.

Pamoja na Uganda kuporomoka nafasi mbili bado imeendelea kuongoza kwa ubora kwa ukanda wa Cecafa ikifuatiwa na Kenya.

Kenya imeshuka kwa nafasi moja hadi 106 ikiwa na pointi 1210.

Sudan imebaki nafasi ya 127 (pointi 1120) huku Rwanda ikipanda kwa nafasi mbili hadi 135 ikiwa na pointi 1094.

Burundi pia imepanda kwa nafasi moja ikiwa na pointi 1085 huku Ethiopia ikibaki nafasi ya 151 ikiwa na pointi 1049.

Sudan Kusini imeendelea kubaki mkiani ikiwa nafasi ya 164 baada ya kukusanya pointi 994.

 

Nafasi 21 za juu hakuna mabadiliko yoyote kwa sababu hakuna nchi iliyocheza mechi za kimataifa kati ya Desemba 2018 na Januari 2019.

Ubelgiji (1727 pointi), Ufaransa (1726), Brazil (1676), Croatia (1634), England (1631), Ureno (1614), Uruguay (1609), Uswisi (1599), Hispania (1591) na Denmark (1589) ndiyo nchi kumi bora.