Stars yapaa, Mkude, Dante nje

Muktasari:

Wachezaji sita wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, wameachwa katika safari ya kwenda Cape Verde kutokana na majeraha. Taifa Stars iliondoka nchini jana usiku kuikabili Vape Verde katika mchezo wa kufuzu fainali za Afrika, unaotarajiwa kuchezwa Ijumaa wiki hii.

Dar es Salaam. Wakati timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ iliondoka jana usiku kwenda Cape Verde kucheza mchezo wa kufuzu Fainali za Afrika, wachezaji sita wameachwa, baada ya kupata majeraha.

Wachezaji waliobaki ni Frank Domayo (Azam), Jonas Mkude (Simba), Andrew Vincent ‘Dante’ (Yanga), Mohammed Abdulrahiman (JKT Tanzania), Salum Kihimbwa na Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar).

Hata hivyo, Domayo ndiye mchezaji pekee aliyecheza mchezo uliopita dhidi ya Uganda, ‘The Cranes’, ambao Taifa Stars ililazimisha suluhu mjini Kampala.

Mkude alipata majeraha katika mchezo ambao Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya African Lyon na siku moja baadaye Dante hakumaliza mechi dhidi ya Mbao FC baada ya kupata majeraha katika ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Yanga. Mechi zote zilichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipa Benedict Tinoco kutoka Mtibwa Sugar, ameitwa katika kikosi hicho.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike alisema ametoa maelekezo kwa wachezaji kujiandaa kukabiliana na shughuli pevu katika mchezo wa Ijumaa unaotarajiwa kuchezwa usiku.

“Tunakwenda Cape Verde tukijua tutakutana na mchezo mgumu kwa sababu wapinzani wetu wana nafasi ya kufuzu, hivyo tutakuwa na kibarua kigumu lakini naamini tutashinda,”alisema Amunike.

Amunike alisema Cape Verde ni timu inayocheza soka ya kiwango bora, lakini Taifa Stars imejiandaa kushindana na itapambana kusaka ushindi dhidi yao.

"Serikali ipo karibu na sisi wamehangaikia kupata usafiri kuhakikisha mambo yote yanakwenda vizuri, tunawashukuru na tunawaahidi hatutawaangusha,"alisema Amunike.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alisema Taifa Stars haitaondoka na ndege mpya ya Serikali Boing 737-8, 'Dreamliner'.

Dk Mwakyembe alisema kukosekana uwanja mkubwa wa kutua ndege hiyo katika mji wanaofikia nchini Cape Verde.

Alisema wamepewa taarifa na watu waliotumwa kwenda kuandaa mazingira kuwa hakuna uwanja wa kutua ndege, hivyo wamebadili ndege itakayokwenda Cape Verde.

Kikosi cha Taifa Stars ni Aishi Manula, John Boko na Shomari Kapombe (Simba), Salum Kimenya (Prisons), David Mwantika, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, Yahya Zaydi na Mudathir Yahya (Azam FC), Ally Abdulkarim na Paul Ngalema (Lipuli).

Wengine ni Beno Kakolanya, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Gadiel Michael, Kelvin Yondani (Yanga), Hassani Kessy (Nkana,Zambia), Abdi Banda (Baroka,Afrika Kusini).

Taifa Stars inaundwa na wachezaji saba wanaocheza soka nje Mbwana Samatta (KRC Genk,Ubelgiji), Himid Mao (Petrojet,Misri), Simon Msuva (Al Jadida,Morocco), Rashid Mandawa (BDF,Botswana), Farid Mussa na Shabani Chilunda (Tenerife,Hispania) na Thomas Ulimwengu (Al Hilal,Sudan).