Stars yaingia kambini, Samatta kutua kesho

WACHEZAJI wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' wameanza kuingia kambini leo Jumatatu Oktoba 5, 2020 kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi huku Nahodha wa timu hiyo Mbwana Samatta anatarajia kuwasili nchini kesho Jumanne.

 

Stars itacheza mechi hiyo ambayo ipo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka duniani (FIFA), Oktoba 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

 

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Cliford Ndimbo amesema jumla ya wachezaji 25, walioitwa na kocha mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije wanatarajiwa kuwa sehemu ya kambi hiyo ambapo wengi wao wameingia kambini kuanza kujifua.

 

Pia nyota wa timu hiyo wanaocheza soka la kulipwa wameanza kuwasili kwa ajili ya kujianda na mchezo huo ambapo Ally Msengi anayecheza Stellenbosch ya Afrika Kusini amewasili huku Thomas Ulimwengu anayekipiga TP Mazembe ya DR Congo akitarajiwa kufika mchana wa leo Jumatatu.

 

Samatta anayeichezea Fenerbahce inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki anatarajiwa kuwasili kesho Jumanne, wakati Himid Mao kutoka Misri, Simon Msuva na Nickson Kibabage wanaocheza Morocco wakitarajiwa kuwasili keshokutwa Jumatano.

 

Stars wameweka kambi yao hoteli ya Tiffan Diamond ambapo mazoezi wanayafanya Uwanja wa Taifa ama Uhuru.

 

Mchezo wa mwisho uliozikutanisha timu hizo mbili ulikua ni wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar uliochezwa Septemba 8, 2019  Uwanja wa Mkapa ambapo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, ambapo iliamuliwa kwa mikwaju ya penalti na  Stars kuibuka mshindi kwa penalti 3-0.