Stars waiachia deni Serengeti Boys

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Mirambo alisema ushindi wa bao 3-0 walioupata Taifa Stars umewapa deni kubwa kwani wao ni wenyeji wa Fainali za Afcon za vijana zinazotarajiwa kufanyika Aprili mwezi ujao jijini Dar es Salaam.

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ Oscar Mirambo amesema wanadeni kubwa kwa Watanzania baada ya Taifa Stars kufuzu Fainali za Afrika (AFCON).

Akizungumza na Mwanaspoti, Mirambo alisema ushindi wa bao 3-0 walioupata Taifa Stars umewapa deni kubwa kwani wao ni wenyeji wa Fainali za Afcon za vijana zinazotarajiwa kufanyika Aprili mwezi ujao jijini Dar es Salaam.

Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Stars na kuweka wazi sasa mtihani umebaki upande wao huku akiwaomba Watanzania kuendelea na hamasa kama ilivyokuwa kwa Taifa Stars.

“Watanzania sasa wanahamia kwetu wanatamani kuona hatuwaangushi tunaendeleza mazuri waliyoyafanya wenzetu hilo linawezekana kikubwa ni ushirikiano tutafika tunapopataka,”

“Vijana wako vizuri wanatamani kuwathibitishia watanzania kuwa wao wanaweza na wana vipaji vya kuifikisha nchi mbali zaidi ya hapa ilipo hivyo kikubwa ni umoja na ushirikiano ili tufikie mafanikio,” alisema.

Alisema wachezaji wameonyesha utayari kushindana katika fainali hizo kwani wanafuata maelekezo ninayowapa siku hadi siku.

Mirambo alisema wachezaji wake wanaonyesha dhamira ya kupambana na wameahidi kufanya vizuri zaidi ili kuendelea kuipa heshima nchi yao.