Stars waanza Tizi kuivaa Burundi

Muktasari:

Wachezaji 19 kati ya  25 walioitwa na Mwalimu Ettiene Ndayiragije ndio wameanza rasmi mazoezi leo Jumanne, Oktoba 6

 Jioni ya leo Jumanne, kikosi cha timu ya Taifa Tanzania “Taifa Stars” kimeanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi  utakaofanyika Jumapili  kwenye uwanja wa Benjamini  Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mazoezi hayo yameanza majira ya saa 10 jioni ambapo yamehudhuliwa na wachezaji 19, kati ya  25 walioitwa na kocha mkuu wa timu hiyo Ettiene Ndayiragije.

Metacha Mnata, Aishi Manula, David Kissu, Shomari Kapombe, Israel Patrick, Mohamed Hussein, David Bryson, Abdallah Kheri, Idd Mobby, Jonas Mkude, Idd Seleman, Salum Abubakari, Said Ndemla, Ditram Nchimbi, Feisal Salum, Dickson Job, Mzamiru Yassin, Bakari Mwamnyeto na Ally Msengi ndio wachezaji waliokuwepo kwenye mazoezi hayo.

Wachezaji hao walianza kwa kufanya mazoezi mepesi ya kukimbia kwa makundi manne kwenye maeneo maalumu huku wakielekezwa na kocha wa viungo.

Baada ya hapo walinyoosha viungo kisha kuanza kucheza mpira kwa makundi staili maarufu kama 'zubaisha bwege' ambapo kila kundi walikua wakikaba wachezaji wawili wawili na kila baada ya dakika zisizopungua  tano walinyoosha viungo na kuendelea na  zoezi hilo.

Walipomaliza  zoezi hilo kocha Ndayiragije aliwagawa kwa makundi mengine mawili ambapo makipa, viungo washambuliaji, mawinga na mastraika walikaa upande wa goli wakati viungo wakabaji na mabeki wote walikaa peke yao upande mwingine.

Mbinu mbali mbali za kukaba, kumiliki mpira na kufunga ziliendelea kuelekezwa na kocha Ndayiragije na wachezaji walionekana kuzielewa na kuzifuata kwa umakini.