Stars mpya ni vita ya makipa

 KOCHA mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amepangua safu yote ya ulinzi ya timu hiyo katika uteuzi wa jana kujiandaa na mechi dhidi ya Burundi Jumapili ijayo.

Ettienne alitangaza kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa huku mabeki wa kati kukiwa na maingizo mapya wakiwemo Iddi Mobby kutoka Polisi Tanzania na Dickson Job wa Mtibwa Sugar ambao watasaidiana na Bakari Mwamnyeto (Yanga) na Abdallah Sebo wa Azam.

Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, huku timu hiyo ikiingia kambini keshokutwa Jumatatu.

Aggrey Morris ambaye ameongoza safu ya ulinzi ya Azam kucheza michezo minne ya ligi bila kuruhusu bao hayupo kikosini.

Kuhusu maingizo mapya kama Iddi Mobby, Dickson Job na Abdallah Sebo, Etienne alisema amewaita ili kuwapa uzoefu na kuwaamini.

“Kuna wachezaji wapya nimewajumuisha katika kikosi na ni baada ya kuridhishwa na uwezo wao katika timu zao wakati ligi inaendelea.Ninachoomba tuwape sapoti ili waendelee kujiamini na naamini kabisa wataisaidia timu,”

Kikosi kikichotangazwa ni Aishi Manula (Simba), Metacha Mnata (Yanga), Davis Kissu (Azam), Shomary Kapombe (Simba), Israel Mwenda (KMC), Mohamed Hussein (Simba), Brayson David (KMC ), Bakari Mwamnyeto(Yanga), Abdallah Sebo (Azam), Dickson Job (Mtibwa), Iddy Mobbi (Polisi Tanzania).

Wengine ni Jonas Mkude (Simba), Himid Mao (Enppi sc ya Misri), Simon Msuva, Nickson Kibabage (Diffa El Jadid ya Morocco), Ditram Nchimbi, Feisal Salum (Yanga), Ally Msengi (Stellenbosch, Afrika Kusini), Mbwana Samatta (Fenerbahce, Uturuki), John Bocco, Said Ndemla na Mzamiru Yassin (Simba), Idd Seleman ‘Nado’ na Salum Abubakar ‘Sure Boy’(Azam).

WADAU WANASEMAJE

Baada ya uteuzi huo wadau mbalimbali wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusiana na uchaguzi huo, ambapo kocha wa zamani wa Toto African, John Tegete alisema; “Wapo baadhi ya wachezaji ambao naona hawakustahili kuwepo kutokana na nafasi zao kwenye timu walizotokea, mfano huyo Ndemla, ukiachana na msimu huu uliopita alicheza chache, sasa huyo katumia kigezo gani.”

“Lakini pia ndani ya kikosi cha Stars sio lazima wachaguliwe wachezaji wa ligi kuu ama watoke Simba na Yanga, wawachukue hata wale wa Ligi Daraja la Kwanza ili wapate nafasi yakuonyesha viwango vyao,” alisema Tegete.

Naye straika wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema anamshauri kocha awe na kikosi mseto kwa ajili ya kuwa na timu endelevu kwa miaka inayokuja, ambao watakuwa wanarithi nafasi za wakongwe.

“Kuna wachezaji kama kina Zawadi Mauya ambao wameshaonyesha uwezo wao, aanze kuwapa nafasi lakini kila wakati kikosi kinakuwa ni kilekile, inaweza ikawa changamoto mbele ya safari, ila kikosi sio kibaya na hayo ndio maoni yangu,” alisema Chambua.

Sept 08 Mwaka jana Stars iliing’oa Burundi katika mechi ya mchujo wa kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa 2022 kwa mikwaju ya penalti. baada ya sare ya 1-1.