Stars inajiamini kinoma Afcon

Muktasari:

Tanzania  imerejea katika fainali za mataifa ya Afrika baada ya miaka 39 kupita, mara ya kwanza kushiriki ilikuwa mwaka 1980 nchini  Nigeria.

KOCHA  msaidizi wa timu  ya taifa ya  Tanzania, Hemed Morocco amesema michezo miwili  ya kirafiki waliyocheza dhidi ya Misri na Zimbabwe imewaimarisha kuelekea mechi ya kesho Jumapili watakayocheza na Senegal katika fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’.
Stars ilicheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Misri ambao walipoteza bao 1-0, katika mchezo huo Stars ilicheza kwa kujilinda zaidi.
Mchezo wa pili walitoka sare ya bao 1-1 na Zimbabwe ambao walikuwa wa  kwanza kupata bao kupitia Knox Mutizwa, nahodha wa Stars, Mbwana Samatta alisawazisha bao hilo.
Morocco  anaamini wamefanya maandalizi ya kutosha kupitia michezo hiyo ya kirafiki hivyo wanaweza kukabiliana na Senegal pamoja na  Algeria wenye aina ya soka linalofanana.
“Kuna mapungufu ambayo tuliyabaini kupitia michezo hiyo ya kirafiki na tumejitahidi kuyafanyia kazi.
 “Kila timu ambayo imefuzu kwa fainali hizi ni nzuri, tumeona wapi tunashida na tumefanyia kazi namna ya kucheza na wapinzani wetu,” alisema kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar.
Baada ya Stars kucheza na Senegal, mchezo wa pili watacheza na Kenya, Juni 27 kabla ya kumalizia mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Algeria, Julai Mosi.