Stars: Watanzania tumewasikia

MIPANGO ya kikosi cha Taifa Stars kuelekea mechi na Tunisia ni mizito, licha ya kupoteza mechi ya kirafiki na Burundi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam, na hiki ndicho walichonena wachezaji.

Kipa wa timu hiyo, David Kisu alifichua siri nzito ya kocha Ettiene Ndayiragije kwamba kupitia mechi ya kirafiki na Burundi, alikuwa anataka kujua timu inachezaje kabla ya kuwakabili Tunisia, hivyo anaamini kuna kitu kinakwenda kufanyika.

Alisema kocha ameshaona mchezaji gani anafaa kucheza na nani, wapi kuna upungufu ili kuweka sawa kukabiliana na Tunisia kufuzu Fainali za Mataifa Afrika (Afcon), dhidi ya Tunisia - mechi itakayopigwa ugenini, Novemba 13.

“Japokuwa kufungwa kunaumiza sana, mbaya zaidi mbele ya mashabiki ambao wana imani na sisi, lakini itatusaidia kutujenga mapema kujua nini tufanye kuelekea mchezo ambao ni muhimu zaidi kwetu,” alisema Kisu

“Bila shaka kocha amejua nini afanye kabla ya kuwakabili Tunisia, tukiwa na uimara wa kila safu, hivyo inawezekana kushinda ugenini huo ndio mpira, kikubwa Watanzania wasivunjike moyo waendelee kutuunga mkono,” alisema Kisu.

Kisu ambaye ni kipa namba moja kwenye kikosi cha Azam FC, na alibahatika kuanza kikosi cha kwanza dhidi ya Burundi akiwaweka nje Aishi Manula (Simba) na Metacha Mnata (Yanga), alisema alifurahia kupewa nafasi itakayomjenga zaidi kiuwezo hasa kwenye michuano ya kimataifa.

“Najua nimekutana na makipa wenye ushindani kwenye kikosi hiki cha Stars, pia wanaanza kwenye timu zao, hilo linaniimarisha kuwa makini na kujituma kwa bidii kuhakikisha kiwango changu kinakua siku hadi siku kwa faida ya Taifa langu na timu yangu ya Azam.”

Naye straika wa timu hiyo, Saimon Msuva alisema mpira wa miguu una matokeo ya kufungwa, kushinda na sare anavyoamivipo kwa ajili ya ushindani wa kufanya wajitume kwa bidii kwa lengo la kufanya vyema mechi iliyo mbele yao.

“Ni matokeo machungu kwetu, lakini hatuna budi kukubaliana nayo ili kufanya vyema mechi yetu na Tunisia itakayopigwa Novemba 13, kwani hata upungufu utakuwa umerekebishwa,” alisema.

Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Morocco katika klabu ya Difaa El Jadida, alisema matokeo na Burundi yatawaongezea umakini wa nini wafanye na sio kuwafanya warudi nyuma zaidi kisa wamefungwa.

beki wa timu hiyo, Dickson Job alisema licha ya kufungwa katika mchezo huo, lakini ana imani kubwa watashinda dhidi ya Tusinia, hivyo wanajipanga vilivyo kuona Watanzania wanafurahia timu yao. “Wachezaji ni kama askari, hatutakiwi kupoa eti kisa tumefungwa, muda wote tupo vitani, tunarekebisha upungufu kisha tunasonga mbele kujua nini tufanye kwenye mchezo uliopo mbele,” alisema.