Stars: Jamani njooni Taifa tuwamalize Sudan

Muktasari:

Taifa Stars inaikabili Sudan katika mchezo ambao kiingilio cha chini kitakuwa sh 2000

WACHEZAJI wa Taifa Stars wamewaita mashabiki kesho Jumapili kuwapa morali ya kufanya vizuri katika mchezo wao dhidi ya Sudan utakaofanyika Uwanja wa Taifa kuanza saa 1:00 usiku.
Taifa Stars itapambana na Sudan katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) na mshindi wa jumla wa mchezo huo atafuzu moja moja.
Kipa wa timu hiyo Juma Kaseja amesema mchezo huo utakuwa mgumu kwani ni hatua za mwisho kuelekea kufuzu hivyo lazima wapambane waweze kushinda.
Kaseja amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono kwani uwepo wao utakuwa chachu ya wao kufanya vziuri.
"Haitakuwa mechi rahisi kwani ni hatua ya mwisho kuelekea Chan hivyo lazima kila timu itataka kupata matokeo mazuri. Tumejiandaa kupata matokeo mazuri na kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kwa kupata ushindi," alisema Kaseja.
Naye beki Gadiel Michael amesema uwepo wa mashabiki wengi utawarahisishia kazi wachezaji kwani watapata morali ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.
"Tunawashukuru mashabiki kila mara wamekuwa wakituunga mkono na safari hii tunawaomba waje kwa wingi kutusapoti kwani uwepo wao ni morali tosha kwetu ya kufanya vizuri"alisema Gadiel.