Stars, Burundi mambo yote kwa Mkapa

Muktasari:

Baada ya zaidi ya mwaka mmoja kupita bila timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kucheza, kiu ya Watanzania na mashabiki wa soka nchini leo itamalizwa kupitia mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10 jioni.

Dar es Salaam. Baada ya zaidi ya mwaka mmoja kupita bila timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kucheza, kiu ya Watanzania na mashabiki wa soka nchini leo itamalizwa kupitia mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10 jioni.

Huenda ikawa ni mechi ya kuvutia kutokana na kufanana kwa mbinu na staili ya kiuchezaji kwa timu hizo kulingana na namna ambavyo zimekuwa zikicheza katika michezo iliyopita.

Timu hizo zimekuwa zikipendelea soka la pasi fupifupi zinazotokea mara kwa mara kutoka kwa viungo na kwenda pembeni ambako ndiko hupatumia kujenga mashambulizi.

Wakati huo zinajenga mashambulizi, mchezaji anayecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati (namba tisa), husogea jirani zaidi na lango la adui, jambo ambalo huwalazimisha walinzi kusogea nyuma ambalo hutoa fursa kwa wenzake hasa mchezaji anayecheza nyuma ya mshambuliaji huyo kunasa mipira katika eneo hilo na kutengeneza nafasi au kufunga.

Katika kufanyia kazi staili hiyo, upande wa Taifa Stars, wamekuwa wakimtumia zaidi nahodha Mbwana Samatta kusimama kama mshambuliaji wa kati, huku Saimon Msuva akicheza nyuma yake kutokana na kasi na wepesi wake wa kusimama na kufika katika nafasi sahihi pindi wanaposhambulia.

Kwa Burundi, nahodha wao Saido Berahino anayecheza soka la kulipwa katika timu ya Charleroi inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji ndiye wanamtumia mara kwa mara kamamshambuliaji wa kati na nyuma yake husimama Cedric Amissi mwenye uwezo wa kufumania nyavu na kuchezesha timu.

Uthibitisho wa namna timu hizo zinavyocheza soka linalofanana ni matokeo ya mechi zilizozikutanisha nyuma ambapo zilionekana kutokuwa na utofauti mkubwa kwani zimekutana mara 11, Tanzania ikishinda mara tano, Burundi mara tatu na sare tatu.

Hata hivyo, Burundi ni wababe kufumania nyavu pindi wakutanapo na Stars kwani wamefunga mabao 12 katika mechi hizo huku Stars ikipachika mabao 11.

Ni mechi ya kwanza ambayo Stars itacheza bila uwepo wa angalau mchezaji mmoja kati ya watatu wanaocheza nafasi ya ulinzi Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na Aggrey Morris ambao wote hawajajumuishwa kikosini.

Wakati Taifa Stars ikimkosa nahodha msaidizi John Bocco ambaye ni majeruhi, Burundi hawatakuwa na mshambuliaji Fiston Abdulrazak ambaye amezuiwa na klabu yake ya ENPPI inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Mechi hiyo kwa kila timu mbali na kutumika kusaka nafasi ya kupanda katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), pia ni kipimo kujiandaa na mechi za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Cameroon, mwakani.

Kwenye viwango vya ubora, Stars iko katika nafasi ya 134 wakati Burundi ipo nafasi ya 149. Wakati Taifa Stars ikijiandaa kwa mechi mbili za kuwania kufuzu Afcon 2021 na Tunisia kati ya Novemba 9 hadi 17, mwaka huu, Burundi itakuwa na mechi mbili dhidi ya Mauritania.

Kwa upande mwingine, mechi hiyo itatumiwa na Stars kama sehemu ya maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), zitakazofanyika mwakani huko Cameroon.

Akizungumzia pambano hilo, nahodha wa Burundi, Berahino alisema wamekuja kucheza kwa nia ya kushinda. “Tunafahamu Tanzania ni timu kubwa yenye uzoefu ambayo imecheza pamoja kwa muda mrefu wakiongozwa na washambuliaji hasa nahodha wao, hivyo tumejiandaa kukutana nao na naamini tutapata ushindi,” alisema Berahino.

Kocha wa Burundi, Ndayizeye Djimi alisema kutimia kwa kikosi chake alichokiita kumempa matumaini ya kufanya vyema katika mchezo huo.

“Tanzania ni nchi ambayo tuko kama ndugu. Tumepata mechi za kirafiki kama tatu, ila tumechagua tucheze na Tanzania. Tumecheza nao kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, hivyo tumekuja kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huu ingawa tunafahamu tunacheza na timu nzuri,” alisema Ndayizeye.

Kipa wa Stars, Aishi Manula alisema wanaipa uzito mkubwa mechi hiyo ingawa ni ya kirafiki. “Kwa niaba ya wachezaji kiujumla tumejiandaa vizuri na tuko tayari kupambana na majirani wa Burundi. Kama mnavyofahamu kwamba mara zote tunazocheza na majirani huwa ni mechi zenye ushindani, lakini kwa pamoja tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kushinda kwa sababu mechi hiyo itatufanya tuone tuko kwenye namna gani kuelekea kwenye michezo inayofuata. Kiujumla tunawaomba mashabiki na Watanzania waweze kujitokeza kwa wingi na kuisapoti timu,” alisema Manula.

Kocha msaidizi, Selemani Matola alisema mchezo huo utakuwa kipimo kwa Stars kutokana na ubora wa Burundi pamoja na uwepo wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi zao waliomo katika vikosi vya timu hizo.

“Haitakuwa mechi rahisi ukizingatia kwamba Burundi tuliwatoa kuwania kufuzu Kombe la Dunia.”