Stand United yawafungia nyota wake wawili

Muktasari:

Stand United imepanga kusajili wachezaji watano kwenye dirisha dogo la usajili. Wamepanga kusajili washambuliaji wawili, mabeki wawili na kipa mmoja.

Dar es Salaam. Stand United 'Chama la Wana' imewafungia wachezaji wake wawili Tariq Seif na Sixtus Sabilo kwa makossa ya utovu wa nidhamu na kuomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubariki adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa wengine.

Mwenyekiti wa Stand United, DK Ellyson Maeja alisema mchezaji Tariq amefungiwa mwaka mmoja na Sabilo aliyefungiwa miezi sita.

Dk Maeja alisema wachezaji hao walionyesha utovu wa nidhamu kwa timu hivyo wanaiomba TFF ibariki adhabu hiyo ili kuwapa fundisho wachezaji wengine kujiepusha na utovu wa nidhamu.  

 "Sixtus alitoroka kambini Oktoba 26 huku akijua siku mbili baadae tuna mchezo wa wapinzani wetu wakubwa Mwadui wakati Tariq ligi ilivyomalizika msimu uliopita alienda Dar es Salaam na hakurejea tena kujiunga na timu. Tulipowasiliana naye hakufanya hivyo na tukamuandikia barua na kusubiri ndani ya siku 14 bado hakutokea hivyo tumefanya uamuzi" alisema Dk Maeja.

Wakati huo huo; Dk Maeja amesema wanahitaji kusajili washambuliaji wawili, mabeki wawili na kipa mmoja katika dirisha dogo la usajili ambalo tayari limeshafunguliwa.

"Tunahitaji kukiimarisha kikosi chetu ikiwemo kusajili wachezaji watano kutoka katika nafasi ya ushambuliaji, beki na kipa ili mzunguko wa pili tuwe vizuri zaidi"alisema Dk Maeja.

Stand United iko nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza michezo 14, imeshinda minne, imetoa sare michezo miwili na imepoteza michezo nane.