Stand United hofu tupu FDL

Muktasari:

Stand United wamebakiza mechi nne dhidi ya timu za Rhino Rangers,Arusha FC,Mawenzi Market na Sahare All Stars ambapo kwa sasa wana pointi 22 na wako nafasi ya 10 katika msimamo wa kundi B.

 

STRAIKA wa Stand United,Miraji Salehe amewatonya wachezaji wenzake kuwa wanatakiwa kukomaa ili kuweza kuibakisha daraja timu hiyo kwani kwa sasa wako katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

 Timu hiyo yenye maskani yake katikati ya mji wa Shinyanga hadi sasa wameshacheza mechi 18 wakiwa nafasi ya 10 wakiwa na pointi 20 ambapo Gwambina wanaongoza na alama zao 40.

Stand United wamebakiza mechi na Rhino Rangers,Arusha FC,Mawenzi Market na Sahare All Stars ambazo mmoja watacheza nyumbani na mitatu iliyobaki watacheza ugenini.

Akizungumza na Mwanaspoti Online,Salehe(19) alisema pasipo kupambana timu hiyo itashuka daraja jambo ambalo litakuwa baya kwao na wadau wa soka wa Shinyanga.

“Salama yetu ni kukomaa na kupata ushindi katika mechi hizi Nne zilizobakia zaidi ya hapo tutaishusha daraja hii timu kitu ambacho kwangu sitaki kukiona,” alisema Salehe ambaye alisajiliwa na Chama la Wana akitokea Pamba FC.

Alisema sasa wanachotakiwa ni kukomaa na kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi Nne zilizobaki ambazo nazo ni ngumu kutokana na kucheza na timu ambazo nazo ziko katika janga la kushuka daraja.

Hadi sasa Straika huyo ameshafunga mabao Nane katika Ligi Daraja la Kwanza ambapo Jacob Masawe wa Gwambina anaongoza akiwa amefunga 10 huku Ramadhani  Athumani wa Rhino Rangers akifunga Tisa.