Stamina kipaumbele Simba ikiiwinda Vita

Muktasari:

Wachezaji wa Vita walionekana kuwa na stamina na nguvu zaidi kulinganisha na wale wa Simba ambao walijikuta wakichoka katika dakika za mwanzoni mwa mchezo huo.

Dar es Salaam. Katika kile kinachoonekana kujifunza kutokana na makosa, benchi la ufundi la Simba limeonekana kutilia mkazo zaidi kujenga stamina ya wachezaji kabla ya mechi yake ya Jumamosi dhidi ya AS Vita.

Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo ambao Simba ilifungwa mabao 5-0 jijini Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wachezaji wa Simba walionekana kuzidiwa mara kwa mara pindi walipokuwa wanawania mpira na wachezaji wa Vita jambo lililochangia wapoteze mchezo huo.

Wachezaji wa Vita walionekana kuwa na stamina na nguvu zaidi kulinganisha na wale wa Simba ambao walijikuta wakichoka katika dakika za mwanzoni mwa mchezo huo.

Katika mazoezi ya Simba yanayoendelea kwenye uwanja wa Boko Veteran, timu hiyo imetumia muda wa saa moja kufanya mazoezi ya stamina tofauti na kipindi kingine ambacho hufanya mazoezi ya namna hiyo kwa muda wa nusu saa kisha kufanya mazoezi ya kimbinu.

Mazoezi hayo ya stamina yalisimamiwa na kocha wa viungo wa Simba, Adel Zrane ambaye alikuwa akiwapa ya aina tofauti kuanzia saa 10 hadi saa 11.

Baada ya mazoezi hayo ya stamina, saa moja iliyobakia, Simba waliitumia kufanya mazoezi ya mbinu uwanjani