Stam awatuliza Biashara United

Muktasari:

  • Kocha wa timu hiyo, Amri Said ‘Stam’ alisema licha ya hali kuwa sio nzuri hawajakata tamaa na kujipa matumaini ya kufanya vizuri mechi zilizobaki.

MWANZA.BIASHARA United inajikongoja kwenye Ligi Kuu kwani haina matokeo mazuri lakini benchi la ufundi pamoja na kukiri mambo kuwa mazito limesisitiza ishu ya kushuka daraja haipo kwani ligi haijaisha.

Timu hiyo imepoteza mechi yake juzi mkoani Shinyanga baada ya kupigwa na Mwadui mabao 2-1, imekusanya pointi 23 inashika nafasi ya 19 huku ikiwa imecheza mechi 26 na kama haitashtuka huenda ikarudi Ligi Daraja la Kwanza.

Kocha wa timu hiyo, Amri Said ‘Stam’ alisema licha ya hali kuwa sio nzuri hawajakata tamaa na kujipa matumaini ya kufanya vizuri mechi zilizobaki.

Alisema timu hiyo inaweza kubadili matokeo hayo endapo safu ya ulinzi itaongeza umakini kwani safu ya ushambuliaji ina uwezo mkubwa wa kushinda ingawa kulinda ushindi ndiyo tatizo kubwa.

“Ligi inaendelea hatuwezi kukata tamaa mapema hivi, tatizo mabeki wanashindwa kulinda ushindi kwa sababu muda mwingine tunatangulia kupata bao lakini tunasawazishiwa na kufungwa,” alisema Stam.

Aliongeza benchi la ufundi litaendelea kupambana kuyafanyia kazi mapungufu yanayojitokeza ili mechi zinazofuata wapate matokeo mazuri na kujinasua na janga la kushuka daraja.

“Benchi la ufundi linaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyopo ili kumaliza ligi nafasi nzuri, kikubwa mashabiki wetu wasikate tamaa,” alisema.