Sportpesa yazitaka Yanga, Simba kamili SportPesa Cup

Muktasari:

  • Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo miaka miwili iliyopita Gor Mahia ya Kenya imefanikiwa kunyakuwa ubingwa huo mara mbili

Dar es Salaam. Magwiji ya soka ya Tanzania, Yanga na Simba wamethibitisha kutumia wachezaji wao wa vikosi vya kwanza katika mashindano ya SportPesa Cup yaliyopangwa kuanza Januari 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas wakati wa kuitangaza kampuni ya MultiChoice Tanzania (DStv) kupewa haki ya kutangaza mashindano hayo mubashara kupitia huduma za vifurushi mbalimbali.

Tarimba alisema kuwa wamekuwa na vikao na viongozi wa timu hizo kuhusiana na ushiriki wao katika mashindano hayo na hasa baada ya matukio ya mashindano ya kombe la Mapinduzi ambapo timu hizo ziliwakilishwa na baadhi ya wachezaji wa timu za pili.

Alisema kuwa mashindano ya SportPesa Cup ni makubwa na yenye zawadi kubwa pia yameingizwa katika kalenga ya mashindano ya Shirikisho la Kandanda la Tanzania (TFF) na hivyo yanahitaji kuthaminiwa.

“Gor Mahia na timu nyingine za Kenya zimethibitisha kuleta wachezaji wao wa vikosi vya kwanza, akina Dennis Oliech watakuja hapa mara baada ya kucheza mechi yao ya marudiano ya kombe la Shirikisho, naamini Yanga na Simba nazo zitafanya hivyo hivyo kwani mashindano haya ni makubwa, yenye zawadi kubwa na  mshindi atacheza na timu yenye historia kubwa Duniani, Everton, lazima vikosi vya kwanza vitumike,” alisema Tarimba.

Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Tanzania, Jacqueline Woiso alisema kuwa wamejipanga kuonyesha michezo hiyo kuanzia kifurushi cha Bomba mpaka Premium na kuwaomba mashabaiki wa soka kuungana nao katika mashindani hayo.

Woiso alisema kuwa wanatarajia kuona timu za Tanzania zinatumia mashindano hayo vizuri kwa kuleta udhindani na kupata nafasi ya kutwaa ubingwa ili kucheza na timu maarufu ya Everton ya Uingereza.

Michuano hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam itashitikisha timu nane za soka kutoka Tanzania na Kenya. Mbali ya Yanga, Simba na Gor Mahia, timu nyingine ni Mbao FC, Singida United zote za Tanzania ambapo kutoka Kenya ni  AFC Leopard, Bandari FC na  Kariobangi Sharks.