Spika Ndugai, Majaliwa kuipa mzuka Stars huko Misri

Muktasari:

  • Taifa Stars inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya pili inayotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 ikipangwa Kundi C pamoja na Kenya, Algeria na Senegal.

Dodoma. Wiki tatu na ushei kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 kuanza, Spika Job Ndugai na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wameahidi kwenda kuwapa mzuka Taifa Stars katika mashindano Afcon itakayofanyika Misri.

Ndugai na Majaliwa wamepania kwenda kuishangilia Stars inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya pili inayotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19 ikipangwa Kundi C na Kenya, Algeria na Senegal.

Jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika bungeni, Spika Ndugai alitoa matangazo yanayohusu michezo akisema Bunge limeanza kuratibu majina ya wabunge wanaotaka kwenda kushuhudia michuano hiyo.

“Bunge linaendelea kuratibu ule utaratibu wa Bunge kwenda Misri tukiongozwa na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Spika mwenyewe,” alisema Spika Ndugai huku akishangiliwa na wabunge

“Ni vyema wabunge tukaonyesha mfano, tukajiandikisha kwa wingi na huu utaratibu unapaswa kufanyika haraka kwa kujiandikisha kwani kule hoteli zitajaa na wabunge tukijitokeza kwa wingi kuishangilia tutafanya vizuri na hata kunyakua kombe,” alisema

Spika Ndugai alitumia fursa hiyo kuipongeza timu ya Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2018/19 baada ya kuinyuka Singida United mabao 2-0, mchezo uliopigwa juzi uwanja wa Namfua mkoani Singida.

“Tunawapongeza Simba kuibuka mabingwa, hongereni sana Simba. Wale wanaoutafuta ubingwa waendelee,” alisema Spika Ndugai huku wabunge wakishangilia

“Hongereni sana Yanga kwa juhudi za kuongoza ligi kwa muda mrefu,” alisema

Kauli hiyo iliwafanya wabunge kushangilia huku sauti ikisikika ikitoka ‘wa mbeleko ya chuma’ na nyingine ‘ubingwa wa TFF.’

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti maalum (CCM) Amina Mollel alilitaka Bunge kutoa tamko la kumpongeza mchezaji wa kimataifa, Mbwana Samatta kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania nje ya nchi.

Samatta ameiwezesha timu yake ya KRC Genk kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji 2018/19.

Mollel aliomba mwongozo akimtaka mchezaji huyo ambaye ni Nahodha wa Stars akisema mchango wa Mtanzania huyo unapaswa kuthaminiwa na kujaliwa hata ndani ya Bunge ili kumtia moyo.

Alisema magoli (20) aliyoifungia timu hiyo kwenye ligi ndiyo imewezesha timu yake huku akiitaka Serikali kukemea kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii cha Samatta kutambulishwa kama raia wa Kenya akitaka jambo hilo likemewe.

Akitoa mwongozo wa Mollel, Spika Ndugai alisema Serikali imesikia na kuwa jambo hilo ni muhimu hivyo Serikali iangalie namna ya kumtaja shujaa huyo.