Sonso aitega Yanga kimtindo

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Sonso alisema; “Leo (jana Jumatatu) ndiyo nimepokea simu ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika kwa mara ya kwanza, tuliongelea mambo ya mkataba wangu.

ZIKIWA zimebaki siku 11 ili dirisha dogo la usajili kufungwa, beki wa Lipuli FC na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars.’ Ally Mtoni ‘Sonso’ amesema hajafanya mazungumzo na Yanga ila yupo tayari kuzungumza endapo atafuatwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sonso alisema; “Leo (jana Jumatatu) ndiyo nimepokea simu ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika kwa mara ya kwanza, tuliongelea mambo ya mkataba wangu.

“Aliniuliza mkataba wangu unamalizika lini nilimwambia na baada ya hapo akasema atawasiliana na uongozi wa timu yangu na maongezi yetu yaliishia hapo hakuna lolote ambalo liliendelea na sijawasiliana naye tena.

“Bado nina mkataba na timu yangu kama watakubaliana na viongozi nipo tayari kwenda kucheza timu yoyote kwani, mpira ni kazi yangu lakini akili yangu kwa sasa ni kuitumikia Lipuli maana ndio waajiri wangu,” alisema Sonso.

Kwa upande wa Nyika alisema hataweza kuzungumzia lolote la usajili mpaka hapo litakapokamilika, lakini kuhusu kuwasiliana na Sonso kweli alifanya hivyo ila si mazungumzo kuhusu usajili.

“Kweli kumekuwa na taarifa za Yanga kumtaka lakini jambo hilo halijafika kwenye kamati yangu. Nimekuwa nikisikia taarifa zake tu. Kama kweli tutakuwa tunamuhitaji tutafanya mazungumzo na uongozi wa Lipuli,”

“Sonso bado ana mkataba na Lipuli na tunafanya usajili kwa matakwa ya Kocha Mwinyi Zahera na kama atakuwa anamuhitaji kamati yangu itaangalia jinsi gani inaweza kumpata, lakini bado tupo kimya tukisubiri kauli ya mwalimu kwanza,” alisema Nyika.

Katibu Mkuu wa Lipuli, July Leo alisema hakuna kiongozi yeyote wa Yanga ambaye amefika kwao au kuzungumza lolote na wamekuwa wakisikia tu taarifa hizo ambazo hazijawa rasmi.

“Hakuna suala lolote la Sonso kuhitajika na Yanga katika ofisi yetu lakini kama kweli wanamtaka wafanye taratibu zote za kisheria kama kututumia barua rasmi na sisi tutawaita mezani ili kuzungumza nao.

“Tukikubaliana tutawapatia kwasasa ana mkataba na timu yetu,” alisema Leo aliyesisitiza Yanga kuacha kuzungumza maneno matupu.