Solskjaer na haja ya mastaa wa zamani kupewa nafasi Man United

Muktasari:

  • Ni jambo jema sana kwa klabu za England hapa kuanza kuchukua wachezaji wao wa zamani waliopata nao mafanikio, wenye mwelekeo mzuri kikazi na kuwaingiza kwenye bodi zao kwa sababu ukweli ni kwamba watu wengi walio kwenye ngazi za utendaji klabuni hawana uzoefu wa kucheza gemu wala kulielewa kutoka kwenye maono ya wachezaji.

KOCHA mpya wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjær alianza kwa makeke akiwa kocha wa muda, lakini baada ya kuidhinishwa mserereko ukamalizika, akianza na kuchabangwa isivyo kawaida ikiwemo Arsenal iliyomkaribisha kwa kumchapa 2-0. Hiyo ndo Ligi Kuu ya England (EPL).

Juzi hapa walifungwa 1-0 na Barcelona nyumbani Old Trafford ambako enzi za kocha Sir Alex Ferguson ilikuwa ngome isiyopigika. Ni kweli Barca ni timu kubwa na Man United katika kipindi cha pili, hasa dakika za mwisho walicheza vizuri.

Hata hivyo, namna ya upangaji wa kikosi na ‘sub’ alizokuwa akifanya ziliacha watu wakishangaa, na katika kipindi cha kwanza vijana wake walicheza hovyo, mara nyingi wakicheza rafu zisizo za maana.

Mchezaji huyu wa zamani wa Mashetani Wekundu anaonekana mwenye kuiweza kazi yake lakini bado kuna kitu kinampwaya, na pengine ningesema anahitaji msaada wa kuwa na mkurugenzi wa michezo kando yake, na Garry Neville ni mmoja wa wakongwe klabuni akiwa pia amecheza hapo na angeweza kusaidia kwenye eneo hilo, akiwa na uzoefu wa biashara pia. Moja ya mambo muhimu niliyong’amua katika kusomasoma kwangu na kutafiti huku na kule ni umuhimu wa kuwa na mkurugenzi wa michezo kwenye timu. Timu zote za NFL na NBA kule Merakani zina wakurugenzi wa michezo na wamekuwapo kwa miaka mingi, kitu ninachoona sasa ni muhimu kabisa kwenye soka.

Ni jambo jema sana kwa klabu za England hapa kuanza kuchukua wachezaji wao wa zamani waliopata nao mafanikio, wenye mwelekeo mzuri kikazi na kuwaingiza kwenye bodi zao kwa sababu ukweli ni kwamba watu wengi walio kwenye ngazi za utendaji klabuni hawana uzoefu wa kucheza gemu wala kulielewa kutoka kwenye maono ya wachezaji.

Ndivyo ilivyo Old Trafford; kule kwenye bodi wamekaa wazee wale tu na huku chini yupo kocha akihangaika na wachezaji wake, asiwe na uhakika ampange yupi na amwache nani; matokeo yake imekuwa ni lawama juu ya lawama na makandokando mengi yasiyoisha.

Alirithi timu iliyokuwa katika mgawanyiko mkubwa kufuatia Jose

Mourinho kuwaharibu wachezaji, akiwaweka benchi wazuri na kuchezesha ‘wazee’ kisha akagombana na walio nyota na muhimu kama Paul Pogba.

Solskjaer aliingia na kupokewa kama mkombozi na muunganishaji wa mambo, lakini sasa naona bado kuna tatizo pale linalotakiwa kufanyiwa kazi haraka, ikiwa United kweli wantaka kurudi kwenye ule ukuu wao wa enzi za Fergie na kuwa tishio ndani na nje ya nchi.

Ni muhimu sana kwa kocha Solskjær kuwa na uhusiano mzuri na Makamu Mwenyekiti Mtendaji Ed Woodward, kwa sababu kimsingi ndiye husajili wachezaji kwa kuwafuata kwenye klabu zao nje ya nchi, lakini ingekuwa rahisi zaidi kuwa na uhusiano bora kabisa ikiwa pangekuwapo wachezaji wa zamani kama yeye na Neville kwenye bodi ya wakurugenzi na mmoja awe mkurugenzi wa michezo.

Neville ni mfanyabiashara ambaye ameshathibitisha uwezo wake katika kazi hiyo, akiwa na uzoefu kwenye soka na amepata pia kufundisha klabu katika ngazi ya juu ya soka. Anaelewa klabu ndani nje na kipi kinahitajika ili kupata mafanikio endelevu. Ukijizungushia watu wazuri basi ujue kwamba utafanya uamuzi na kuenenda kwenye mazuri.

Tumeona pale Chelsea, hapa jijini London jinsi mambo yamebadilika tangu kuondoka kwa Mkurugenzi wa Michezo, Michael Emenalo. Pale palionekana kuwapo na sera ya uhamisho wa wachezaji iliyokuwa wazi kabisa, ikitaka kuchukua wachezaji chipukizi kama Romelu Lukaku na Kevin De Bruyne, waliosonga na kufanya mambo makubwa.

Emenalo alikuwa mtu aliyehusika sana na usajili wa jinsi hiyo na alikuwa nguvu imara kwa miaka mingi. Lakini alipoondoka, klabu walionekana kupoteza mwelekeo huo. Wazo langu kuu ni kwamba, wachezaji wa zamani waliofanikiwa kwenye klabu wapewe nafasi ya kuwa katika bodi na kusaidia kutokana na uzoefu wao.

Solskjær ameshapewa mkataba wa miaka mitatu wa kuwanoa United,

Zinedine Zidane amerudi Real Madrid huku ukiwakuta wachezaji mahiri wa zamani kama Frank Lampard na Steven Gerrard wakiwa wameanza kazi ya ukocha.

Nashangaa kutowaona akina Solskjærs wengi katika klabu kwa ajili ya kurejesha ‘utukufu’ uliopotea. Anafaa lakini anahitaji mchezaji mwingine wa klabu aongeze nguvu na ushauri pia kwenye masuala ya usajili si kuwaachia wale wazee kwenye bodi.