Solskjaer mambo matamu

Muktasari:

  • Solskjaer amepewa kibarua cha kuinoa Man United kwa muda hadi mwisho wa msimu, lakini baada ya kushinda mechi zote sita alizosimamia timu hiyo, upepo umegeuka na sasa kocha huyo anapendwa kuanzia kwa wachezaji, mashabiki na sasa mabosi kwenye bodi.

MANCHESTER, ENGLAND.OLE Gunnar Solskjaer ameweka jina lake kileleni kabisa katika orodha ya makocha wanaoweza kuteuliwa kuinoa Manchester United moja kwa moja.

Bosi Ed Woodward na mabosi wengine wa Man United wameonekana kuvutiwa na namna kocha huyo wa muda anavyofanya mambo yake tangu alipochukua timu hiyo, ambapo kwenye mechi sita, ameshinda zote.

Makamu mwenyekiti, ambaye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu kocha mpya, Ed Woodward Jumapili iliyopita aliingia kwenye vyumba vya kubadilishia huko Wembley kwenda kumpongeza Solskjaer baada ya kikosi hicho kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspur.

Na sasa Solskjaer yupo nafasi kubwa ya kupewa kibarua cha kudumu, huku kocha pekee anayemnyima usingizi kwenye kukikamatia kibarua hicho ni Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur.

Solskjaer amepewa kibarua cha kuinoa Man United kwa muda hadi mwisho wa msimu, lakini baada ya kushinda mechi zote sita alizosimamia timu hiyo, upepo umegeuka na sasa kocha huyo anapendwa kuanzia kwa wachezaji, mashabiki na sasa mabosi kwenye bodi.

Ushindi huo kwenye mechi dhidi ya Spurs umeifanya United kulingana pointi na Arsenal katika mbio za kukamatia nafasi ya nne ili kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Ole ameichukua United kutoka kwa Jose Mourinho.