Solskjaer kumpa unahodha Pogba

Muktasari:

  • United ina hofu wakala wa Pogba, Mino Raiola tayari ameshazungumza na Madrid kuhusu uhamisho huo katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto.

MANCHESTER, ENGLAND.MANCHESTER United wanatapatapa. Wanapambana. Ni katika kuhakikisha wanambakisha kiungo wao mahiri, Paul Pogba ambaye anatakiwa kwa nguvu zote na Real Madrid. Na sasa wapo tayari kumpa kitambaa cha unahodha ili abakie Old Trafford.

Tayari Manchester United imeshamwambia staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwamba hatauzwa klabuni hapo licha ya mwenyewe kuanza kuonekana kuvutika na mpango mzima wa kwenda Real Madrid mwishoni mwa msimu.

Madrid ipo tayari kutoa kitita cha Pauni 100 milioni kwa ajili ya Pogba ambapo kocha wa Madrid, Zinedine Zidane amemfanya kuwa miongoni mwa mastaa wachache wakubwa anaowataka mwishoni mwa msimu huu na ameweka hadharani kwamba anavutiwa na kiwango cha staa huyo Mfaransa mwenzake.

United ina hofu wakala wa Pogba, Mino Raiola tayari ameshazungumza na Madrid kuhusu uhamisho huo katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto.

Lakini sasa United imeongeza mbinu za kumbakisha baada ya kuamua kumpa kitambaa cha unahodha mwishoni mwa msimu huu huku pia wakimuongeza mkataba mwingine ambao utamfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi kikosini.

Nahodha wa United, Antonio Valencia anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu pindi mkataba wake utakapomalizika na United waliamua kutomuongezea mkataba mpya na sasa kocha, Ole Gunnar Solskjaer anatazamiwa kuwa na nahodha mwingine msimu ujao.

Kwa sasa beki wa pembeni, Ashley Young ambaye ni mchezaji mkongwe zaidi klabuni amekuwa akivaa kitambaa hicho kutokana na Valencia kusugua benchi. Hata hivyo, Pogba, David De Gea na beki Chris Smalling nao wamevaa kitambaa hicho katika nyakati tofauti.

Lakini Solskjaer anataka sasa Pogba afuate nyayo za wakongwe maarufu wa zamani kama Bryan Robson na Roy Keane kuvaa kitambaa cha unahodha wa timu hiyo.

Solskjaer ametiwa nguvu na mazungumzo aliyofanya na Pogba katika siku za karibuni baada ya kumpa mipango yake ya baadaye huku akitaka yeye ndiye aendeshe kikosi cha United ndani ya uwanja huku akiwa na kitambaa begani.

Maamuzi ya Solskjaer yanakuwa tofauti na maamuzi ya kocha aliyepita United, Jose Mourinho ambaye aliwahi kumpa unahodha msaidizi Pogba lakini akaamua kumvua kitambaa hicho Septemba mwaka jana siku moja baada ya United kutolewa katika michuano ya Kombe la Ligi na Derby County.

Kabla ya hapo Pogba ambaye alitwaa ubingwa wa dunia na kikosi cha Ufaransa Julai mwaka jana nchini Russia alikuwa amekosoa hadharani mbinu za kocha huyo Mreno akitaka United icheze soka la kushambulia zaidi na si kujihami.

Mourinho alitangaza maamuzi ya kumng’oa Pogba katika nafasi yake huku akikanusha kwamba wawili hao walikuwa katika bifu zito kama ilivyokuwa inaripotiwa na waandishi wa habari mara kwa mara.

“Hapana. Ukweli pekee ni kwamba nimeamua Paul asiwe nahodha msaidizi tena. Lakini hakuna ugomvi. Hakuna matatizo kabisa.

Mtu yule yule aliyeamua Paul asiwe nahodha msaidizi ndiye mtu yule yule aliyeamua Paul awe nahodha msaidizi. Mimi mwenyewe,” alisema Mourinho wakati huo.

“Mimi ni kocha, nafanya maamuzi haya. Hakuna ugomvi wala tatizo lolote. Ni maamuzi fulani ambayo sihitaji kuyatolea maamuzi,” aliongeza kocha huyo wa zamani wa Chelsea, Inter Milan, Porto na Real Madrid ambaye anajulikana kwa ukorofi wake dhidi ya mastaa mbalimbali aliowahi kuwafundisha.

Mastaa wengine waliowahi kuwa manahodha kwenye kikosi cha Manchester United kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990 achilia mbali Bryan Robson na Roy Keane ni pamoja na Steve Bruce, Eric Cantona, Gary Neville, Nemanja Vidic, Wayne Rooney.