Solskjaer atuliza mzuka Man United

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesisitiza kwamba mchezaji wake ambaye amesajiliwa katika dirisha hili la usajili lililopita, Donny van de Beek atacheza katika kikosi cha kwanza kwa dakika zote kwenye michezo ijayo, hiyo ni baada ya kuingia akitokea benchi katika mchezo dhidi ya Newcastle.

Van de Beek ambaye amecheza kwa dakika 59 tokea ajiunge na miamba hiyo dirisha lililopita amekuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaoingia kutokea benchi lakini anaonesha kuwa na msaada mkubwa katika timu pale anapopata nafasi.

“Amecheza kwenye mchezo wa leo (juzi), ni miongoni mwa wachezaji bora katika kikosi, nafikiri mumemuona akiwa anacheza kwenye mechi na mazoezini, sio mwepesi kupoteza mpira,”alisema.

“ kwa sasa nahitaji kupata uwiano katika timu ndio maana kuna mabadiliko mengi kwenye timu na mnaniuliza kwanini sijamuanzisha mchezaji ambaye nilimuingiza baadae na akaonesha kuwa na matokeo chanya kutokana na uwepo wake kwenye timu, hivyo ilikuwa ni mipango yangu lakini anaweza kuanza katika timu zijazo,”aliongeza Solskjaer.

Van De Beek ambaye alisajiliwa kwa Pauni 40 milioni alianza kufunga katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Crystal Palace ambapo Man United ilipoteza.

Manchester United kwa sasa inashikilia nafasi ya 14 kwenye msimamo wa EPL, huku mchezo ujao ikiwa na kibarua kizito dhidi ya washindi wa pili wa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya PSG katika mchezo wa hatua ya makundi wa michuano hiyo na baada ya hapo itakuwa na shughuli pevu mbele ya Chelsea katika muendelezo wa Ligi Kuu England.